KAGAME AZUNGUMZIA UWEZEKANO WA KUTOKEA VITA KATI YA RWANDA NA UGANDA


Rais wa Rwanda, Paul Kagame amepuuza uwezekano wa nchi yake kuingia vitani na Uganda, ingawa amesisitiza kuwa nchi hiyo jirani inafadhili waasi wa nchi yake.

Kagame amesema hayo katika mahojiano na Gazeti la Taz la Ujerumani, wakati wa mkutano wa kimataifa jijini Brussels, Ubelgiji na kunukuliwa na The Daily Monitoe la Uganda.

Katika majibu yake kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi katika uhusiano wa nchi hizo jirani, Kagame alisema “Watu wanahofia vitana baina yetu (Uganda na Rwanda). Sioni kama kuna vita vinakuja kati yetu, nadhani Uganda inajua gharama zake. Hatutaki kwenda chini katika njia hiyo kwa kuwa kila mmoja atapoteza kitu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu onyo la vita alilolitoa kwa Uganda Aprili, Rais Kagame alijibu: “Ndiyo, (vita vitatokea) ikiwa utavuka mpaka.

"Unaweza kufanya chochote unachotaka ndani ya himaya yako, kama kukamata watu. Lakini ukivuka mpaka wetu na kutaka kufanya mambo ndani ya himaya yetu – hicho ndicho nilichomaanisha.”

Rwanda imekuwa inaituhumu Uganda kwa kuwakamata watu wake na kuwashikilia wakati mwingine ikiwa kimya na bila kuwafungulia mashtaka, jambo ambalo Kagame alilieleza gazeti la Ujerumani kuwa halikuwa zuri.

Alisema Uganda ingelitumia sheria zake kumshtaki Mnyarwanda yeyote anayekamatwa badala ya kuwashikilia kwa muda mrefu kwa madai ya kuifanyia ujasusi na baadaye kuwaachia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post