Kaka wa kambo wa Kiongozi wa Korea Kaskazini aliuawa baada ya kubainika kuwa ni jasusi wa shirika kuu la kijasusi la Marekani CIA.
Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, Kim Jong-nam, kaka wa kambo wa Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un aliuawa kwa sumu akiwa safarini nchini Malaysia mwaka 2017.
Gazeti hilo limechapisha ripoti hiyo Jumatatu na kusema limedokezewa hayo na mtu mwenye taarifa kamili kuhusu tukio hilo. Gazeti hilo limedokeza kuwa, kulikuwa na mawasiliano baina ya CIA na Kim Jong-nam.
Uchunguzi uliofanywa na Malaysia kuhusu kesi hiyo mwaka jana uligundua kuwa, kaka wa kambo wa Kiongozi wa Korea Kaskazini alikutana an raia mmoja wa Marekani, aliyeshukiwa kuwa ni jasusi, katika hoteli moja nchini Malaysia siku nne kabla ya kuuawa tarehe 9 Februari 2019.
Kabla ya hapo, raia mmoja wa Indonesia Siti Aisyah na raia mmoja wa Vietnam, Doan Thi Huong walikuwa wamekamatwa kwa tuhuma za kumpa sumu Kim Jong-nam katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur, lakini waliachiliwa huru mapema mwaka huu nchini Malaysia baada ya kukosekana ushahidi.
Marekani na Korea Kaskazini zina historia ndefu ya uhasama na uadui. Mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani alikutana na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un nchini Singapore kwa ajili ya mazungumzo ya nyuklia.
Walifanya mkutano wa pili mjini Hanoi Vietnam mapema mwaka huu lakini mazungumzo hayo yaligonga mwamba baada ya Korea Kaskazini kuituhumu Washington kuwa imepoteza fursa nadra ya kupunguza uhasama.
Social Plugin