Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, VIJANA, AJIRA AHIMIZA USHIRIKIANO KWA WATUMISHI


Na; Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe amewaasa watumishi wa ofisi hiyo kufanyakazi kwa ushirikiano ili waweze kutumiza malengo waliyojiwekea.


Hayo ameyasema wakati alipokutana na watumishi wa ofisi yake Dodoma kwa lengo la kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23 kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kuonesha mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni;

“Uhusiano kati ya uwekezaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Jenga utamaduni wa Utawala bora, matumizi ya TEHAMA na Ubunifu katika utoaji wa huduma jumuishi.”

Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ipo kisheria Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Ofisi hiyo ina majukumu makubwa ya kiutendaji hivyo watumishi wanawajibu wa kufanyakazi kwa kushirikiana na kujenga umoja.

“Ushirikiano katika kazi ni muhimu na husaidia kuboresha mifumo ya kiutendaji ikiwemo kuwa na mikakati endelevu ya ofisi, mawasiliano mazuri, kujenga mahusiano mazuri na wadau na kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Massawe.

Sambamba na hilo aliwasihi watumishi wa ofisi hiyo kufanyakazi kwa bidii, weledi, uzalendo na kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao na utoaji wa huduma kwa wadau na wananchi.

Pia amewashauri watumishi hao kuepukana na vitendo vya rushwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na maadili ya Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia haki na usawa.

Aidha, Katibu Mkuu alikutana na kufanya kikao na wadau mbalimbali wa nje na alipokea maoni na mrejesho wa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Waziri kuhusu sekta ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Ajira, Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Hifadhi ya Jamii na masuala ya Vyama vya Wafanyakazi.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Peter Kalonga aliafiki yaliyosemwa na kuahidi kuahidi kufanyia kazi maagizo hayo ikiwemo suala la ushirikiano na mawasiliano katika utendaji kazi baina ya watumishi ili kuimarisha mshikamano baina ya watumishi.

Kwa upande wake alisema kuwa kikao hiko kimewezesha watumishi wa ofisi hiyo kubadilishana taarifa zaidi za kiutendaji na kitasaidia kuimarisha ushirikiano baina yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com