Mkazi wa Mbezi, Vicent Marseli (37), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam, akikabiliwa na shtaka la kumshika sehemu za siri mtoto wa miaka mitatu ili kujiridhisha kimapenzi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Neema Moshi, alidai Februari 18 eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alifanya shambulio la aibu kwa kumshika mtoto huyo sehemu za siri ili ajiridhishe kimapenzi.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na mwendesha mashtaka wa Jamhuri alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.
Hakimu Kiliwa alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaotoa bondi ya Sh 50,000 kila mmoja.
Hata hivyo, alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa Juni 25, mwaka huu.
Social Plugin