Kundi linalojiita dola la Kiislam kwa mara ya kwanza limedai kuhusika na uasi nchini Msumbiji lakini wataalam wametilia shaka madai hayo na polisi ya Msumbiji imepuuza taarifa hiyo.
Uasi wa makundi ya itikadi kali umekuwa ukiongezeka katika jimbo la kaskazini ya Msumbiji la Cabo Delgabo tangu mwaka 2017 ambapo zaidi ya watu 200 wameuwawa na vijiji kuchomwa moto.
Kulingana na kampuni moja inayofuatilia shughuli za makundi ya itikadi kali, kundi la IS limelitoa taarifa yake hapo jana likidai kuhusika katika makabiliano ya bunduki na jeshi la Msumbuji yaliyotokea hivi karibuni katika jimbo la Cabo Delgado.
Wapiganaji wa itikadi kali wamekuwa wakivishambulia vijiji na kuua watu mara kwa mara licha ya uwepo wa askari wengi wa polisi na jeshi katika jimbo hilo linalopakana na Tanzania.
Polisi ya Msumbuji imepuuza madai hayo ya kundi la IS yaliyotolewa wakati Waislam duniani wanasherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Social Plugin