NA SALVATORY NTANDU
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linaendelea kuwatafuta Majambazi wawili waliotelekeza silaha aina ya Gobole iliyotengenezwa kienyeji,panga mmoja pamoja na pikipiki aina ya SANLG yenye namba za usajili MC 359 AZE baada ya kushindwa kutekeleza tukio la uporaji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea jana katika mtaa wa shunu saa tatu na nusu usiku ambapo walilenga kufanya uhalifu katika duka la M pesa la Neema Byabato mkazi wa shunu wilayani Kahama.
Amesema wakati polisi wakiwa katika doria walipata taarifa za kuwepo kwa tukio hilo kisha kuanza kuwafuatilia Majambazi hao walipobaini kuwa wanatafutwa walianza kukuimbia na katika harakati za kukimbia walidondosha silaha hizo na kisha kuitelekeza pikipiki hiyo.
Amesema Majambazi hao walikuwa na lengo la kumpora fedha Neema baada ya kufunga duka lake lakini hawakuweza kufanikiwa baada ya njama yao kuharibiwa na jeshi la Polisi na Juhudi za kuwatafuta zinaendelea ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Pikipiki hiyo na silaha hizo zimehifadhiwa katika kituo cha polisi Wilaya ya Kahama.
Social Plugin