Afisa wa polisi anayehudumu katika kituo cha Riruta nchini Kenya amepuliziwa dawa na kuibiwa silaha yake na washukiwa wa ujambazi.
James Obiri alikutwa amelala kando ya barabara ya Mtamba katika mtaa wa Highridge karibu na kituo cha polisi cha Parklands.
Kulingana na ripoti iliyoandikishwa Riruta mnamo Alhamisi, Juni 20,2019 Obiri alikuwa amepoteza fahamu na hakuweza kuzungumza wakati alikimbizwa katika hospitali ya Avenue ili kufanyiwa uchunguzi wa matibabu.
"Maafisa wa polisi waliomtembelea walimpata akiwa amelazwa baada ya kupelekwa hospitalini humo akiwa hali mahututi na maafisa wa polisi wa Parklands. Afisa huyo alipewa dawa aina ya opioid kulingana na uchunguzi wa madaktari," ripoti hiyo ilisema.
Baadaye alisafirishwa hadi hospitali ya Nairobi West ambako anaendelea kupokea matibabu.
Bastola yake iliyokuwa na risasi 14 iliibwa. Hata hivyo hii sio mara ya kwanza kwa maafisa wa polisi kupoteza silaha zao mikononi mwa wahalifu.
Jumanne, Aprili 16, majambazi walivamia kituo cha polisi kaunti ya Nandi na kuiba bunduki tatu wakati maafisa waliokuwa wakishika doria walikuwa wameenda kutazama mechi.
Chanzo- Tuko
Social Plugin