MAKAMBA ARIDHISHWA NA KASI YA UZALISHAJI WA MIFUKO MBADALA

Na Lulu Mussa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba amefanya ziara ya kikazi ya kukagua viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala ikiwa ni siku ya nne tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Marufuku ya Mifuko ya Plastiki nchini.

Akiwa katika Kiwanda Cha African Paper Bag Ltd kilichopo katika eneo la Chango’mbe jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema ameridhishwa na kasi ya kiwanda hicho ambacho kinazalisha mifuko ya karatasi laki tano kwa siku na mifuko ya ‘Non-Woven’ ipatayo laki moja kwa siku.

“Wajibu wa Serikali si kupiga marufuku na kuondoka, tunahakikisha tunaziba pengo la mifuko ya plastiki kwa kuweka mazingira wezeshi kwa uzalishaji wa mifuko mbadala yenye ubora na bei nzuri kwa watu. Lazima tuwasaidie wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viwanda kuzalisha mifuko ili kuziba pengo la mahitaji kwa kuwa na mifuko mbadala yenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji” Makamba alisisitiza.

Amesema kuondoka kwa mifuko ya plastiki kumeibua fursa mpya za uchumi shirikishi, ajira mpya, mapato mapya na kusisitiza kuwa Shirika la Viwango Nchini (TBS) linaandaa viwango vipya vya ubora wa mifuko hiyo mbadala vitakavyobainisha malighafi na unene wa mifuko mbadala itakayozalishwa ili kuwalinda watumiaji ikiwa ni pamoja na taarifa zitakazoainisha mfuko husika una uwezo wa kubeba kilo ngapi.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kampuni ya African Paper Bag Ltd Bw. Hasnai Mawji amesema kuwa kwa sasa mahitaji ya mifuko kiwandani kwake ni makubwa sana na wameongeza uzalishaji kwa kuagiza mashine mpya mbili sambamba na kuongeza idadi ya watumishi kukidhi mahitaji kwa sasa.

“Kiwanda chetu kinazalisha mifuko tani 100 kwa mwezi na tumeagiza mashine nyingine ili kuongeza uzalishaji wa kufikia tani 200 kwa mwezi na sasa tunafanya kazi masaa 24, shifti zimeongezeka kutoka shifti 1 ya awali na sasa tuna shifti 3, tumeongeza ajira kutoka watu 30 awali na sasa tuna watumishi 60 na lengo ni kufika watumishi 100” Alilisitiza Bw. Mawji.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba pia amepata fursa ya kutembelea Kiwanda cha Green Earth Paper Product Ltd kilichopo katika eneo la Mbezi Makonde chenye uwezo wa kuzalisha mifuko 22,000 kwa siku na kusisitiza kuwa katazo la mifuko ya Plastiki si kwa faida ya mazingira pekee bali pia ni muhimu katika kuinua uchumi na ustawi wa watanzania.

Aidha Mkurugenzi wa Kiwanda cha Green Earth Paper Product Bw. Robert Mosha amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya zuio kiwanda hicho kilipokea oda ya kiasi cha Shilingi Milioni 124 na katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya zuio la mifuko ya plastiki kiwanda hicho kimepokea mahitaji yenye thamani ya Shilingi 124 ikiwa ni kiwango cha juu ukilinganisha na mahitaji ya awali kwa kipindi kifupi.

Kuanzia tarehe 1 Juni Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki nchini ikiwa ni pamoja na Utengenezaji, Uingizaji, Usambazaji, Usafirishaji na Matumizi ya Mifuko hiyo bila kujali unene wake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post