Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametimiza ahadi yake ya kuwazawadia wachezaji wa Simba waliotwaa tuzo za mwaka za klabu hiyo zilizopewa jina la ‘Mo Simba Awards’ zilizofanyika wiki iliyopita Hyatt Regency, Dar es Salaam.
Sambamba na wachezaji hao, wakiongozwa na kipa Aishi Manula, pia Makonda alimpa zawadi ya kipekee nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta kwa kuupa mtaa jina la mshambuliaji huyo.
Wachezaji wa Simba waliokabidhiwa zawadi hizo za fedha taslimu Dar es Salaam jana ni Manula aliyeondoka na sh milioni 10 kama kipa bora aliyeng’ara msimu huu, huku wengine wakiwa ni Meddie Kagere (mfungaji na mchezaji bora) na Erasto Nyoni (beki bora).
Wengine ni Clatous Chama (bao bora), James Kotei (kiungo bora), John Bocco (mshambuliaji bora), Rashid Juma (chipukizi bora) ambao kila mmoja alipata sh milioni moja.
Pia, Makonda alimzawadia sh milioni mbili mchezaji bora wa timu ya wanawake ya Simba, Simba Queens, Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’, huku pia akimpa sh milioni tatu Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara kwa kuthamini mchango wake katika uhamasishaji.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Makonda alisema: “Nimetaka kukamilisha ahadi nilioahidi siku ya Tuzo Mei 30 zilizoandaliwa na kupewa jina la MO Simba Awards 2019 ambazo hutolewa kwa wachezaji wa Simba Sport Club kila mwaka.
“Kubwa ni kutambua mchango na kujituma kwa mchezaji wa Simba aliyechaguliwa na wachezaji wenzake ni Erasto Nyoni aliyeshinda tuzo mbili na beki bora, wakati Meddie Kagere akiibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia namsifu Kagere kwa kuwaaminisha watu na staili yake ya kufumba jicho moja,” alisema Makonda.
Aidha, Makonda Alitumia nafasi hiyo kumpa Samatta zawadi ya mtaa kwa heshima aliyoipa Tanzania huko Ulaya, akiibuka mfungaji bora wa Genk, lakini pia kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ubelgiji.