Elizabeth Mmari (20), mkazi wa kijiji cha Kilingi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujaribu kumuua mwanaye.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 12, 2019 na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Siha, Jasmine Abdul, baada ya kuridhika na ushahidi wa watu wanne uliotolewa mahakamani hapo.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, David Chisimba amedai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimnywesha mtoto wake sumu aina ya dipu, Novemba 2,2018.
Amesema alimpa sumu hiyo akidai kushindwa kumlea baada ya mwanaume aliyempa ujauzito kumkimbia.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo mwendesha mashtaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kikatili dhidi ya watoto. Mtoto alinyeshwa sumu hiyo siku tatu baada ya kuzaliwa.
Na Babati Chume, Mwananchi
Social Plugin