Mke wa baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amelazwa katika Hospitali jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini jana Jumatano Juni 5, 2019 akitokea Kampala Uganda alipokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.
Mtoto wake Makongoro Nyerere amesema, baada ya kuwasili nchini mama yake alipumzishwa kwa muda wakati madaktari wakiendelea na uchunguzi kabla ya kufikia uamuzi wa kumlaza.
Makongoro alisema alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Kampala nchini Uganda alikokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.
Mama Maria Nyerere alikuwa nchini Uganda kwa ajili ya ibada maalum ya kukumbuka mchango wa hayati Mwalimu juliasi Nyerere kwa Afrika na Ukristo.
Tangu mwaka 2009, waumini wa kanisa katoliki wamekuwa wakifanya ibada katika hekalu la Namugongo kwa ajili ya kumkumbuka mwalimu Nyerere.
Nyerere alitoa mchango mkubwa sana kwa ajili ya kuung'oa madarakani utawala wa rais Idi Amin..