Marekani imeanza kuchukua hatua za kuiondoa Uturuki kutoka mpango wa kuunda ndege za kivita chapa F-35 ikilenga Julai 31 iwe tarehe ya mwisho kwa Uturuki kuwa sehemu ya mpango huo.
Hayo ni kwa mujibu wa barua iliyochapishwa jana kutoka kwa kaimu waziri wa Ulinzi wa Marekani Patrick Shanahan kwenda kwa mwenzake wa Uturuki Hulusi Akar.
Hatua hiyo imekuja baada ya Uturuki kusisitiza kwamba itaendelea na mipango yake ya kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kutoka Urusi uamuzi ambao umeikasirisha Marekani.
Kwenye barua hiyo, Shanahan amearifu Uturuki kuwa bado inayo nafasi ya kubadili uamuzi na kufafanua hatua zaidi ambazo Marekani inalenga kuchukua katika wiki zijazo.
Kwa kuanza, Uturuki haitoalikwa kwenye kikao kuhusu ndege chapa F-35 kitakachofanyika Ubelgiji wiki ijayo,na marubani wa Uturuki wanaoshiriki mafunzo ya kutumia ndege hizo wanapaswa kuondoka Marekani katika kipindi cha wiki saba zijazo.
Social Plugin