Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBARONI KWA KUMTUKANA MATUSI HADI KUFA MAMA YAKE MZAZI


Na Peti Siyame, Nkasi 

POLISI wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa inamshikilia William Sokoni (33) akidaiwa kumtukana matusi ya nguoni, mama yake mzazi, Clemensia Wangabo (77) na kumsababishia umauti.

Mwanaume huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mtenga inadaiwa alighadhabika baada ya mama yake mzazi kumtaka amlipe kiasi cha Sh 50,000 alizomkopesha muda mrefu.

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, wilaya ya Nkasi kwa masharti ya mtoaji taarifa kutoandikwa majina yake gazetini kwa kuwa sio msemaji wa jeshi hilo zimethibitisha kutokea kwa mkasa huo uliotokea Juni 10, mwaka huu katika kijiji cha Mtenga, Kata ya Mtenga wilayani humo.

Diwani wa Kata ya Mtenga, Pacras Maliyatabu akizungumza na gazeti la Habarileo kuhusu mkasa huo katika mji mdogo wa Namanyere, alisema kuwa maziko ya mama huyo yalifanyika juzi kijijini humo.

“Mama huyo kwa muda mrefu alikuwa akimdai mwanawe, William na kumtaka kiasi cha Sh 50,000 alizomkopesha... mke wa William alimsihi mumewe amlipe mama yake na kweli mumewe alikubali na kumpatia apeleke,” alieleza. 

Aliongeza kuwa baada ya mke wa William kufika nyumbani kwa mama mkwe wake ili alipe deni hilo, ghafla William alitokea nyumbani hapo na kuanza kumporomoshea matusi mama yake mzazi.

“Alimtusi mama yake kuwa heri yeye William angenyonya maziwa ya mbwa kuliko ya mama yake huyo, ndipo ghafla mama huyo akaanguka na kupoteza fahamu mbele ya mwanawe huyo na mkewe,” alieleza Malyatabu.

Akizungumza na gazeti la Habarileo kwa njia ya simu, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mtenga, Daina Namfukwe alisema kuwa Clemensia alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika zahanati hiyo.

Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com