Mwanafunzi wa stashahada ya maabara kutoka Chuo Kikuu cha Kampala tawi la Tanzania (KIU), Anifa Mgaya amefariki dunia jana Jumapili usiku baada ya kushambuliwa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.
Anifa alikutwa na umauti majira ya saa 2 usiku jirani na geti la kuingia katika chuo hicho kilichopo Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam alichokuwa akisoma.
Taarifa zinaeleza baada ya kushambuliwa, wanafunzi wenzake walijitokeza ili kumpatia msaada kwa kumkimbiza hospitali lakini hadi wanafika alikuwa tayari umauti umemfika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akibainisha vijana waliohusika katika tukio hilo wanasemekana kuwa ni vibaka.
“Marehemu alikuwa anatoka kujisomea chuoni, wakati akitoka muda huo karibu na geti alikutana na vijana hao wawili waliokuwa wanajaribu kumpora begi lakini baada ya kusumbuana walimchoma kwa kutumia kitu chenye ncha kali na taarifa kamili ya tukio hilo itatolewa kesho,” amesema Chembela.
Na Aurea Simtowe,Mwananchi
Social Plugin