Mwanaume aitwaye Shija Mahoiga (45) mkazi wa kijiji cha Igaga "A" wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa kwa kutumia kipande cha chuma na Raphael Martine ( 34) baada ya kumfumania akiwa amelala na mke wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Richard Abwao aliyoitoa kwa vyombo vya habari,tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa Juni 21,2019 majira ya saa tisa alfajiri katika kitongoji cha Mwasele "B" mji mdogo wa Mhunze kata ya Kishapu wilaya ya Kishapu.
“Raphael Martine mkazi wa Mhunze – Kishapu alivunja mlango na kumshambulia mgoni wake Shija Mahoiga kwa kutumia kipande cha chuma, sehemu za kichwani, miguuni, mikononi na kwenye mbavu za kushoto”,ameeleza Kamanda Abwao.
“Chanzo cha tukio ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumfumania Shija Mahoiga akiwa amelala na mke wake aitwaye Maria Kija ambaye nae amejeruhiwa na amelazwa katika hospitali ya Jakaya – Kishapu”,ameongeza.
Kamanda Abwao amesema mtuhumiwa amekamatwa huku akitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuacha kujichukulia sheria mkononi na waheshimu sheria za nchi.Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin