BENKI YA AKIBA YAKABIDHI VIFAA VYA USAFI KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA 2019

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 05, 2019, benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) imekabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza ili kuimarisha huduma ya usafi sokoni hapo.


Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imeambatana na zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu jijini Mwanza ambapo wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika pamoja na wafanyabiashara sokoni hapo kufanya usafi huo.

Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na zoezi endelevu la kufanya usafi katika soko hilo na kuweka mazingira katika hali ya usafi ili kuzuia magonjwa ya milipuko huku akitoa pongezi kwa Serikali kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella na kuvikabidhi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza, amesema vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa wa kuimarisha usafi na hivyo wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama kiafya.

Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola ameishukru benki ya Akiba kwa kutoa vifaa hivyo na kuomba liwe zoezi endelevu huku akitoa rai kwa wafanyabiashara sokoni hapo kuvitumia vyema kuimarisha usafi kama ilivyo desturi yao ya kufanya usafi kila jumamosi.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki hiyo ili kuimarisha hali ya usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza. Zoezi hilo limeambatana na shughuli ya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi ili kusaidia huduma ya usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza. Hafla hiyo imeambatana na zoezi la usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Vifaa vilivyokabidhiwa na benki ya Akiba ni pamoja na mifagio, mapipa ya kutunzia taka, koleo, reki, buti za usafi, glovusi, toroli na maski.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba. Kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa tatu kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akisoma taarifa fupi kuhusu vifaa vilivyotolewa na benki hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akizungumza kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amehimiza vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba kutumika vyema kuimarisha usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza ambalo amesema miezi michache ijayo litaanza kujengwa upya kuwa la kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamas Nchola akitoa salamu za shukrani kwa benki ya Akiba baada ya kupokea vifaa vya usafi.
Afisa Mazingira (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza), Mangabe Mnilago akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakifanya usafi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani 2019.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiwa kwenye usasi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika na wafanyabiashara katika Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani, Juni 05, 2019.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiendelea na usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) wakiondoa uchafu katika eneo la kukusanyia uchafu lililopo Soko Kuu jijini Mwanza.
HOTUBA YA FUPI YA MENEJA WA TAWI LA MWANZA BI: HERIETH BUJIKU ILIYOSOMWA KATIKA HAFLA YA KUKABIDHI VIFAA VYA USAFI KWA UONGOZI WA SOKO KUU LA MWANZA KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI.



Mheshimiwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza

Uongozi wa Soko la Kuu Mwanza

Ndugu Wanahabari

Wafanya biashara kutoka soko kuu Mwanza

Mabibi na Mabwana

Itifaki ikizingatiwa



Ndugu Mgeni Rasmi

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa ajili ya siku njema ya leo. Nasema ni siku njema kwani sisi kama Benki ya Akiba tumefarijika sana kupata fursa hii ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya usafi katika soko kuu la Jiji la Mwanza.


Soko hili ni kati ya masoko makubwa sana hapa Mwanza na linapokea bidhaa nyingi kutoka sehemu mbali mbali za kanda ya ziwa. Kwa hiyo ni soko ambalo linasaidia kuinua maisha ya wakulima pamoja na kutoa ajira kwa watu mbali mbali. Sisi kama Benki ya Akiba tunao wateja wengi tu tunaowahudumia kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo mikopo ambayo inasaidia kukuza mitaji na kuendeleza biashara za wafanyabiashara mbali mbali katika soko hili.



Ndugu Mgeni Rasmi

Benki ya Akiba inatambua na inathamini mazingira na ni mdau mkubwa katika harakati za kutunza mazingira. Najivunia kusema hilo kwani sera ya Akiba ya huduma za kijamii yaani Corporate Social Responsibility imeweka kipengele cha mazingira kama sehemu mojawapo ambayo Benki itakuwa inashughulikia katika kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoihudumia.



Kwa kudhihirisha hili napenda kusema kuwa Benki inafanya jitihada nyingi katika eneo hili mathalan Benki imechukua jukumu la kuendeleza na kutunza Viunga vya bustani ya Indepence Square vilivyopo jijini Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi yetu. Viunga vipo katika mandhari nzuri kabisa ya kuvutia na vinapendezesha sana muonekano wa jiji la Dodoma. Jitihada hizi zilianza kuanzia mwaka 2013 na napenda kusema kuwa zoezi hili kwetu litakuwa la kudumu na endelevu.



Pia napenda kusema kuwa jitihada zetu za kufanya usafi pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa zoezi endelevu la usafi limedhihirika sehemu mbali mbali kama Soko la Tandale,Buguruni Jiji la Mbeya n.k. Maeneo haya yameweza kufaidika na huduma hii pamoja na kukabidhiwa vifaa vya usafi kwa ajili ya kuhakikisha kuwepo kwa usafi endelevu. Vivyo vivyo kwa leo hapa Soko Kuu Mwanza zoezi hili linahitimishwa kwa kukabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa soko kwa ajili ya matumizi ya baadaye.



Ndugu Mgeni Rasmi

Benki ya Akiba ni Benki ya Kibiashara ambayo imejikita kuhudumia wananchi wa hali ya chini na wa kati kwa lengo la kuboresha maisha yao na kuinua jamii kiujumla. Benki hii inatoa huduma zote za kibenki kama nilivyoainisha hapo mwanzo yaani mikopo, amana mbali mbali, kutuma na kupokea fedha nje na ndani ya nchi. Huduma nyinginezo kama za mawakala wa kuuza na kupokea float zinapatikana na Mawakala wa kuuza float yaani M-pesa, Tigo Pesa, Airtel Money, Halo Pesa n.k wanahudumiwa kwa haraka bila kusimama foleni na wengi wao wameweza kukuza mitaji yao kupitia mikopo tuliyowapa.


Huduma nyingine za kurahisisha upatikanaji wa huduma za Kibenki kupitia simu za mikononi yaani Akiba Mobile inaptika masaa 24 na imeleta faraja na unafuu kwa wateja wetu kwani inarahisisha na kuokoa muda. Wateja wengi wanatumia huduma hii kuweka fedha kwenye akaunti zao, kufanya marejesho ya mikopo pamoja na mahitaji mengi kama kulipia ving’amuzi, LUKU, bili za maji n.k.



Aidha, huduma za kuuza na kununua fedha za Kigeni zinapatikana katika matawi yetu na tunawakaribisha mtutembelee kwa ajili ya mahitaji yenu yote ya kuuza na kununua fedha kigeni. Pia huduma ya E-statement inapatikana; huduma hii inaleta wepesi wa mteja kupata taariza za akaunti yake kwa urahisi pasipo kwenda Benki kupitia simu ya mkononi, kompyuta n.k. Mteja anatakiwa tu aende kwenye tawi lake kuhakiki taarifa zake pamoja na kutoa anuani ya barua pepe au E-mail address.



Manufaa ya huduma ya E-statement hayaishii kwa mteja kwani yanasaidia pia katika utunzaji wa mzingira kwa sababu inapunguza na kuondoa matumizi ya karatasi. Hii pia ni jitihada za Benki za kutunza mazingira inaonyesha jinsi ambavyo Benki ya Akiba ni Rafiki Bora wa mazingira.



Ndugu Wanahabari

Kwa kuhitimsha naomba niwashukuru wote kwa kutuunga mkono katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani amabayo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kupinga Uchafuzi wa Hewa- yaani Air Pollution", sisi kama benki tunauunga na dunia katika hilo kwani tunatambua umuhimu wa kuwa na hewa safi. Takwimu zinasema kwamba 92% ya watu duniani hawavuti hewa safi hili ni tatizo kubwa sana na zinahitajika juhudi za makusudi kwa ajili ya kupambana na tatizo hili kwani linahatarisha afya za watu pamoja na viumbe hai wengine na mazingira kwa ujumla.



Ndugu Mgeni Rasmi

Kwa niaba ya Benki ya Akiba naomba pia nitoe pongezi kubwa kwa Serikali ya awamu ya tano kufuatia juhudi za makusudi za kupiga marufuku matumzi ya mifuko ya Plastiki ambayo kwa kwa kweli inaleta uharibifu mkubwa kwa mazingira. Sisi kama taasisi pia tupo mstari wa mbele katika kutekeleza agizo hili na tunatoa rai kwa wananchi wote hususan wakazi wa Mwanza kuachana na matumizi ya vitu hivi kwa ajili ya kutunza mazingira yetu ili kuhakikisha urithi bora wa vizazi vijavyo.


Mwisho kabisa, naomba nichukue fursa kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi vikiwemo fagio, mapipa ya kutunzia taka, koleo, rake, buti za usafi, gloves, toroli, masks na vingine kwa uongozi wa soko kwa matumizi ya badae. Lengo ni kuhakikisha kuweko kwa zoezi endelevu la usafi katika soko hili kwa ajili ya kutunza mazingira na kuzuia magonjwa ya milipuko. Hili eneo ni muhimu sana kwa jamii kwani mahitaji ya chakula yanapatikana sana katika soko hilo. Kwa umuhimu huo basi naomba uongozi wa soko undelee kutilia mkazo wa usafi katika eneo hili kwani eneo lenye mahitaji muhimu kama haya linahitaji kutunzwa kwa umakini mkubwa.



Asanteni sana kunisikiliza

Herieth Bujiku – Meneja wa Tawi la Mwanza

Akiba Commercial Bank.

Tazama video hapa chini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post