Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : DC MBONEKO AFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO..AKERWA NA DOSARI HALMASHAURI YA SHINYANGA


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kukumbana na dosari ambapo baadhi ya  majengo yameanza kutoa nyufa kabla hata ya kuanza kutumika.


Mboneko amefanya ziara hiyo leo Juni 18,2019 kwa kukagua ujenzi wa madarasa mawili, matundu ya vyoo pamoja na nyumba mbili za walimu katika shule ya msingi Masunula iliyopo kata ya Usule, Shule ya sekondari Itwangi, kukagua madarasa mawili, shule za msingi Tinde “A” na “B” pamoja kukagua madarasa na matundu ya vyoo kwenye shule hizo  na kukumbana na dosari hizo.

Mkuu huyo wa wilaya pia amekagua  huduma za matibabu katika kituo cha afya Tinde.

Mradi mwingine alioukagua ni Skimu ya umwagiliaji iliyopo kata ya Nyida ambapo Mboneko ameagiza ukamilishwe kwa wakati kabla ya mvua kuanza kunyesha mwezi Oktoba mwaka huu, ili wakulima wanufaike kwa kulima zao la mpunga na kuwainua kiuchumi.

Akikagua miradi hiyo ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo, Mkuu huyo wa wilaya alieleza kutofurahishwa na ujenzi wake kutokana na kujengwa chini ya kiwango na tayari majengo yameanza kutoa nyufa kabla hata ya kuanza kutumika na kuagiza dosari hizo zifanyiwe kazi haraka sana.

Alisema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini thamani ya fedha hizo imekuwa haionekani kutokana na miradi yake kujengwa chini ya kiwango matokeo yake inaendelea kuwagharimu kwa kuifanyia marekebisho ya mara kwa mara.

“Nakuagiza Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri, muwe mnakagua miradi hii pale inapojengwa pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu na siyo kuwaachia hawa mafundi pekee (Local Fundi) kufanya kazi peke yao, na kututekelezea miradi chini ya kiwango,” alisema Mboneko.

“Kuna baadhi ya miradi hamjawahi kufika kabisa kukagua hadi inamalizika kujengwa kama ujenzi huu wa madarasa katika shule ya Sekondari Itwangi, hakuna kitu kilichofanyika, jengo lina nyufa huku rangi zake zikipakwa hovyo hovyo tu, hivyo nakutaka usimamie marekebisho yote haya,”aliongeza.

Katika hatua nyingine aliuagiza uongozi wa halmashauri kuongeza idadi ya wahudumu wa afya katika kituo cha afya Tinde baada ya kukuta kuna upungufu mkubwa wa wauguzi, huku akitoa wito kwa wazazi kuwanyonyesha maziwa ya mama watoto wao ili wapate afya njema na kukua kiakili.

Hata hivyo, Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Shinyanga William Lusiu, alikiri kutofika kwenye ujenzi wa  baadhi ya miradi hiyo ya maendeleo, kwa madai ya kukabiliwa na ukosefu wa gari  kwa ajili ya kutembelea miradi, huku akiahidi kusimamia marekebisho yote ya mapungufu ambayo yamejitokeza kwenye ujenzi wa miradi.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog

TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akikagua ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Masunula Kata ya usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini,kulia ni mkuu wa shule hiyo Gladius Kujerwa na (kushoto) ni Mhandisi wa halmashauri hiyo William Lusiu akiandika dosari ambazo zimejitokeza kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akikagua ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi Masunula na kubaini kuwepo na nyufa kwenye majengo hayo huku yakipakwa rangi vibaya.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akiendelea na ukaguzi wa madarasa katika shule ya msingi Masunula.

Ukaguzi ujenzi wa madarasa ukiendelea katika shule ya msingi Masunula.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akiangalia nyufa katika madarasa ya shule ya msingi Masunula.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akikagua utengenezaji wa madawati katika shule ya msingi Masunula na kubaini yametengezwa chini ya kiwango na kuagiza yarekebishwe.

Ukaguzi wa madawati ukiendelea katika shule ya msingi Masunula.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko (wa pili) akikagua ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya Msingi Masunula.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akikagua ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya msingi Masunula.

Ukaguzi wa nyumba za walimu ukiendelea pamoja na utoaji wa maagizo zijengwe kwa kiwango kinachotakiwa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akiendelea na ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Itwangi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko akiangalia nyufa katika ujenzi wa madarasa katika Sekondari ya Itwangi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko akikagua upakwaji wa rangi katika ujenzi wa madarasa ya shule ya Sekondari Itwangi na kuagizwa urudiwe ikiwa yamepakwa rangi vibaya.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa madarasa na madawati katika shule za msingi Tinde "A" na "B".

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akimwonyesha nyufa kwenye ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi Tinde "A" Mhandisi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga William Lusiu.

Ukaguzi wa ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Tinde "A" ukiendelea.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akikagua ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji katika kata ya Nyida na kuagiza ukamilike kwa wakati kabla ya mvua kuanza kunyesha.

Ukaguzi wa Skimu ya umwagiliaji katika kata ya Nyida ukiendelea.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiangalia mtoto aliyezaliwa kwenye kituo cha Afya Tinde.

Awali mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiangalia kitabu cha mahudhurio ili kubaini kama mhandisi wa ujenzi wa halmashauri huwa anahudhuria kwenye kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo na kubainika huwa hatembelei miradi hiyo na kusababisha kujengwa chini ya kiwango.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akitoa maelekezo kwa mhandisi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga William Lusiu, kuwa anatembelea ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa mafundi wa mitaani (Local Fundi) ili kuondoa changamoto ya kujengwa miradi chini ya kiwango.

Awali mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akiwa kwenye ziara ya ujenzi wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kubaini kuwepo na madudu ya miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com