Uganda na Zimbabwe zilitoka sare ya moja kwa moja katika mechi ya kundi A la kinyanganyiro cha kombe la mataifa ya Afrika kinachoendelea nchini Misri.
Uganda ilijipatia bao la mapema kupitia Emmanuel Okwi baada ya mlinda mlango wa Zimbabwe George Chigova kupangua shambulio la Lumala Abdi.
Lakini Zimbabwe ilisawazisha kupitia kwa Khama Billiat alipofunga baada ya kazi nzuri katika wingi ya kushoto iliofanywa na mchezaji Ovidy Karuru.
Katika mchezo mwingine ambao ulipigwa usiku wa kuamkia leo Nyota wa Misri Mohamed Salah alifunga bao moja na kutoa pasi iliosababisha kufungwa kwa bao la pili dhidi ya DR Congo na kuwavusha kuelekea katika raundi ya mtoano ya timu 16.
Misri ilitangulia kufunga baada ya Salah kupenyezewa nzuri na mchezaji wa klabu ya Aston Villa Ahmed Elmohamady ambaye alifunga goli la pili.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool alifunga goli hilo wakati akiwa amezungukwa na wachezaji wawili wa DR Congo baada ya mshambuliaji Trezeguet kumfanyia kazi nzuri.
Misri ambao ni mabingwa mara saba wa kombe hilo sasa wanajiunga na Nigeria katika mechi za mtoano.
Nigeria iliwachapa Guinea bao moja kwa nunge katika mechi ya ufunguzi siku ya Jumatano na kuwa taifa la kwanza kufuzu katika raundi ya mtoano.