Na Petty Siyame- Habarileo
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kirando, Dk Gideon Msaki alisema iliwachukua zaidi ya saa sita kuokoa maisha ya Joyce kufuatia huduma ya dharura ya upasuaji waliyomfanyia ikiwa ni pamoja na kumuongezea uniti nne za damu.
"Naendelea vizuri....nampenda sana mtoto wangu,” anasema kwa taabu Joyce Kilinda (32) anayesadikiwa kurarua tumbo lake kwa ‘wembe’ na kumtoa mtoto wa kike akiwa hai, wakati alipoulizwa na mwandishi kuhusu hali yake juzi.
Mwanamke huyo amehamishiwa hospitali Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga kwa matibabu zaidi. Kuendelea kuimarika kwa hali ya mwanamke huyo kumetokana na juhudi kubwa za saa sita za kuokoa maisha yake zilizofanywa katika kituo cha afya Kirando baada ya kumpokea akiwa hajitambui na kupoteza kiasi kikubwa cha damu.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu, mzazi huyo alifikishwa katika Kituo cha Afya Kirando huku sehemu ya utumbo ukiwemo mfuko wa uzazi na kondo la nyuma vikiwa nje.
Aliongeza kuwa godoro alilobebewa mwanamke huyo kutoka nyumbani kwake hadi kituoni lilikuwa limelowa damu huku mwenyewe akiwa amezimia ambaye amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Rukwa mjini hapa na kupokewa Alhamisi saa tano usiku.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kirando, Dk Gideon Msaki zaidi ya saa sita kuokoa maisha ya Joyce kufuatia huduma ya dharura ya upasuaji waliyomfanyia ikiwa ni pamoja na kumuongezea uniti nne za damu kwa kuwa alikuwa amepoteza damu nyingi.
Joyce na mwanawe wamelazimika kusafirishwa umbali wa kilometa 160 kutoka Kituo cha Afya Kirando hadi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Rukwa mjini hapa, huku hali yake na mwanawe vikielezwa kuimarika.
Dk Kasululu anakiri kuwa hadi sasa bado uchunguzi wa kitabibu haujabaini nini hasa kilichomsibu mwanamke huyo kujirarua tumbo lake na kumtoa mtoto akiwa hai. “Isitoshe swali jingine ambalo halijapatiwa majibu ni kwamba hajathibitishwa kama ni yeye mwenyewe aliyejirarua tumbo lake na kumtoa mtoto nje au kuna mtu mwingine aliyemfanyia hivyo,” alisisitiza.
Timu ya ufuatiliaji ya wataalamu wa afya ngazi ya mkoa na wilaya ikiongozwa na Dk Kasululu imejiridhisha kuwa huduma za dharura za upasuaji wa kuokoa maisha ya mwanamke huyo zimefanyika kwa mafanikio makubwa.
Kuonesha kuimarika kwa afya yake, Joyce ambaye amelazwa katika chumba maalumu cha uangalizi, mwandishi wa gazeti hili alipomtembelea aliweza kuinuka na kuketi kitandani kwa msaada wa muuguzi, Veronica Wambura.
Kituo cha Afya Kirando ambacho kiko umbali wa kilometa 160 kutoka Sumbawanga mjini ni miongoni mwa vituo vya afya tisa ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imevifanyia upanuzi na ukarabati kwa zaidi ya Sh bilioni 4 vikiwa na uwezo wa kukabiliana na huduma za upasuaji wa dharura.