MKUU WA MKOA AMTAKA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA MBULU NA TIMU YAKE WAJITAFAKARI

Mkurugenzi wa  halmshauri ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara Hudson Kamoga, ametakiwa kukaa chini  na timu yake kutafakari na kushauriana njia bora za kuweza kuongeza mapato kwenye halmashauri hiyo. 


Hayo yameelezwa  na mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti katika Baraza la Madiwani la kujadili na kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo halmashauri hiyo imepata hati safi. 

Mnyeti amesema halmashauri hiyo inatakiwa ijikite katika kubuni vyanzo vya mapato kutokana na halmashauri hiyo kuwa na wigo mpana wa kukusanya ushuru pamoja na  mapato kwenye maeneo mbalimbali.  

"Mkurugenzi kaa na timu yako na mjaribu kutafakari, msing'ang'ane sana na mapato ya bil. 1.4 kwani hayatoshi kwenye kutekeleza majukumu yaliyopo kwenye shughuli za maendeleo. 

"Inaonekana hii halmashauri ilikuwa ni shamba la bibi, watu walikuwa wanakuja wanajipigia hela wanaondoka, suala la kusema ilikuja hela ya Afya ikabadilishwa na kwenda kwenye elimu, huu ni uongo kabisa watu walikaa wakaona huku kwenye afya hawawezi kupiga dili wakabasilisha matumizi kupoteza maboya ionekane hela nilienda kwenye elimu kumbe imeliwa hapa katikati. 

"Kwenye Document inaonyesha hii fedha ni ya afya sasa huwezi kuchunguza kwenye afya kwa sababu wanakwambia ni fedha ambayo imebadilishwa matumizi tena wanafanya bila kuwa na kibali cha Serikali kwa sababu unapotaka kubadilisha matumizi ya fedha ni lazima uwe na kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Tamisemi",  alisema Mnyeti. 

Naye mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga amempongeza mkuu wa mkoa kwa kuwa anajiamini lakini pia kwa kuwatetea kwa yale wanayoyasimamia na  kumuahidi kuwa atahakikisha hawapati hati chafu na mapato katika halmashauri yataongezeka. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Joseph Mandoo amesema kwa Sasa halmashauri za mkoa wa Manyara zimepiga hatua kwani awali ni halmashauri mbili tu ndizo zilikuwa zinapata hati safi. 

"Tumepokea maelekezo yako, mimi na baraza langu tutaendelea kusimamia  fedha za serikali na menejimenti na kuhakilisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi",  Alisema Mandoo. 


Na beatrice Mosses - Manyara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post