Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameagiza kupitiwa upya mkataba wa mauziano ya nyumba 4,000 kati ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na wakazi wa Vingunguti, Dar es Salaam.
Uamuzi huo unafuatia kutozingatiwa kwa masharti ya mkataba ulioingiwa awali, ambao umeonekana kuwa na upungufu wa kisheria na hivyo kusababisha PMM 2001 Ltd kushindwa kuwalipa wamiliki wa nyumba katika eneo la Vingunguti kwa karibu miezi tisa kama walivyokubaliana jambo lililozua taharuki.
Dk. Mabula alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, baada ya kukutana na pande zote mbili za kamati inayosimamia makubaliano ya uuzaji nyumba 4,000 katika mitaa minne ya Vingunguti ambayo ni Mnyamani, Mtambani, Mtakuja na Faru, Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli katika ofisi za wizara hiyo, jijini hapa.
Alisema baada ya kupitia mkataba wa mauziano ya nyumba katika eneo la Vingunguti, kati ya PMM 2001 Ltd na wamiliki wa nyumba, wamebaini kutofuata taratibu za kisheria na kubainisha kuwa wamiliki ambao hawajalipwa fedha yoyote hawabanwi na mkataba huo na wanaweza kuzifanyia shughuli yoyote nyumba zao.
Social Plugin