Idara ya Uhamiaji Tanzania imewataka Watanzania wanaotaka kusafiri nje ya nchi hivi karibuni kubadilisha hati zao za kusafiria kabla ya Julai 2019.
Hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza wa kuzuiwa kusafiri kwenye viwanja vya ndege na vituo vya mipakani wakati wa kutoka nje ya nchi.
Taarifa iliyotolewa jana Juni 3, 2019 na kusainiwa na Msemaji wa Idara hiyo, Ally Mtanda imeeleza ni hitaji la kisheria kwa hati za kusafiria kuwa na uhai wa angalau miezi sita ili mwenye hati hiyo aweze kuomba visa ya kwenda nchi nyingine.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa kuhamia katika matumizi ya hati za kusafiria za kielektroniki zilizozinduliwa Februari 1 mwaka 2018 na Rais John Magufuli.
Mtanda ameeleza hati za zamani zitasitishwa matumizi yake Januari 31 mwaka 2020 hivyo ni muhimu kwa wahitaji wa hati mpya kuzipata kabla ya muda huo.
Kuhusu namna ya kupata hati mpya amesema idara hiyo imeshakamilisha ujenzi wa miundombinu katika mikoa 29, ofisi ya uhamiaji makao makuu, ofisi za uhamiaji Zanzibar na ofisi za balozi za Tanzania katika nchi 23.
Na Elizabeth Edward, Mwananchi