Zaidi ya watu 1,000 wanatarajiwa kushiriki mkutano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kufanyika nchini.
Mkutano huo wa 39 unatarajiwa kufanyika Agosti 17 na 18 na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.
Akizungumza na wamiliki na wakuu wa vyombo vya habari nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi jana Jumatano Juni 12, 2019 alisema mkutano huo pia utamtawaza Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa SADC.
Rais Magufuli anachukua nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Rais wa Namibia Hage Geingob ambaye amemaliza muda wake.
Mkutano huo utatanguliwa na vikao vya mawaziri na makatibu wakuu wa nchi wanachama wa SADC na maonyesho ya viwanda yatakayofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kuandaa mkutano wa SADC ilikuwa mwaka 2003 wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Social Plugin