Rais Magufuli amesema mradi wa majengo wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliopo wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam ni mradi bomu na wa kifisadi.
Ameyasema hayo jana wakati akizindua ghala na mitambo ya gesi ya Kampuni ya Taifa Gas iliyoko Vijibweni wilayani Kigamboni.
Rais Magufuli alisema mradi huo ambao ni maarufu kwa jina la Dege, unapaswa kubadilishwa matumizi yake kwa kuwa majengo hayo hayaendelezwi kwa lolote.
“Yale majengo ya NSSF yamekaa kwa muda mrefu na ni mradi bomu, wa ovyo na wa kifisadi. Tumeshawaeleza haya NSSF pamoja na bodi washughulikie, watoe mawazo yao na nyie wananchi mtoe mawazo yenu tuone jinsi gani haya majengo tunaweza kuyatumia katika njia iliyo sahihi.
“‘Investment’ kubwa kama hiyo imekaa na wala hatutoi majibu. Kama ni kuyatoa yawe mabweni ya chuo au nyumba za wafanyakazi tusubiri uchambuzi utakaofanywa,” alisema Rais Magufuli.
Novemba mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alitembelea mradi huo na kusikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaoendelea katika eneo hilo na kuagiza ulinzi uimarishwe.
Mkataba kati ya NSSF na AHEL ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni hodhi ya ‘Hifadhi Builders’ ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45.
Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa katika mradi na asilimia 35 kampuni hiyo ingetakiwa kuweka fedha taslimu.
Mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu Sh trilioni 1.5.
Hadi kufikia Juni mwaka jana, NSSF walishailipa Kampuni ya Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 kama mchango wake katika ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na Sh bilioni 305.8 wakati Kampuni ya Azimio ilitoa Dola 5,500,000 sawa na Sh bilioni 12.6 tu.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Kigamboni kuwa serikali inazifanyia kazi changamoto zao za kukatikakatika kwa umeme na ujenzi wa miundombinu ya barabara ikiwemo barabara ya Kibada-Kimbiji hadi Mji Mwema.
Amesema Mpango Mkuu (Master Plan) wa serikali ni kuifanya Kigamboni kuwa Mji wa Kisasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo uboreshaji na uimarishaji wa miundombinu mbalimbali ni sehemu ya mpango huo.