Rais Magufuli amesema kuwa anatamani wakati atakapomaliza muda wake wa uongozi, Tanzania iwe na mabilionea zaidi ya 100.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika Ikulu ya Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano kati yake na wafanyabiashara kutoka wilaya zote za Tanzania kwa lengo la kujadili changamoto zinazokwamisha sekta hiyo.
Magufuli amesema jambo hilo litamfanya afurahi kuona anamaliza muda wake huku akiacha mabilionea wengi nchini kutokana na kile alichokuwa akikifanya katika kuboresha mazingira ya biashara.
“Thubutuni na msiogope kufanya biashara ya aina yoyote, nchi yetu imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri, rutuba, maji kwa ajili ya uvuvi, mifugo, madini fursa nyingi za uwekezaji zitumieni ili ziwanufaishe ili siku nikiwa naondoka angalau niache wafanyabiashara mabilionea zaidi ya 100, nitafurahi sana.” Amesema.
Rais Magufuli pia ameashiria changamoto za biashara katika mipaka ya nchi hiyo na amewataka wafanyabiashara hao kutumia fursa ya masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Social Plugin