Rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi anatarajiwa kuwasili nchini leo kuanza ziara ya siku mbili.
Akizungumzia ujio huo jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi mchana leo kumpokea Rais huyo wa DRC atakapowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni.
Alisema Rais Tshisekedi anafanya ziara rasmi nchini kufuatia mwaliko aliopewa na mwenyeji wake Rais John Magufuli baada ya kuchaguliwa na wananchi wa DRC kushika wadhifa huo mkubwa.
“Nawaomba wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi ili kumpokea kiongozi huyu ambaye ameonesha mapenzi mema kwetu na kukubali kuja nchini kipindi kifupi tu tangu amechaguliwa kuliongoza taifa la DRC,” alisema Makonda.
Asubuhi kesho Rais huyo atatembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), baadaye atarejea Ikulu kwa mazungumzo na Rais Magufuli. Tshisekedi aligombea kama kiongozi wa upinzani katika uchaguzi uliofanyika Disemba mwaka jana baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila kung’atuka madarakani.
Social Plugin