Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela wa pili kushoto akiwa na diwani wa Mwangata Nguvu Chengula (mwenye suti nyeusi) na viongozi wengine wakimtazama mama wa watoto watatu ambao nusuru wapoteze maisha kwa kukosa huduma ya matibabu
Na Francis Godwin, Iringa
Serikali ya wilaya ya Iringa imepongeza jitihada za diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengula (CCM) za kuokoa maisha ya mkazi wa Mwangata D Amida Mgonakulima na wanae watatu wasife kwa kukosa matibabu baada ya kutelekezwa na ndugu wakiwa nyumbani.
Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard kasesela leo baada ya kuwatembelea wagonjwa hao waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa wakiendelea na matibabu ,kuwa jitihada hizo zilizochukuliwa na diwani huyo ni za kupongezwa kwani bila kufanya hivyo uwezekano wa mwanamke huyo na wanae kupona ulikuwa ni mdogo.
“Nimefarijika sana kuona hali ya wagonjwa hao ikiendelea vizuri maana huyo mama wa watoto alianza kuoza kuanzia kiunoni kushuka chini na hakuwa na uwezo hata wa kusimama kitandani lakini kwa sasa afya yake inazidi kwenda vizuri hakika diwani Chengula kanusuru uhai wao “ alisema Kasesela .
Aidha alitoa agizo kwa viongozi wa serikali za mitaa katika wilaya ya Iringa kufanya msako nyumba kwa nyumba ili kujua watoto ama wagonjwa waliotelekezwa kwa kukosa huduma za matibabu.
“ Yawezekana kabisa wagonjwa hao ni baadhi tu ya wagonjwa wengi ambao wamefungiwa ndani bila kutibiwa sasa naagiza watendaji wa mitaa kupita nyumba kwa nyumba kukagua na kama kuna nyumba mlango utakutwa umefungwa fungueni kagueni ndani mkiwa na mwenye nyumba ili kujua ndani kuna nini “ alisema Kasesela.
Kasesela alisema tukio jingine kama hilo la Mwangata la mgonjwa kutelekezwa amelisikia kijiji cha Kisanga na amekwisha tuma watendaji kwenda kufuatilia na kuwa matukio yote hayo ni ya kikatili na hatakubali kuyasikia ama kuyaona ndani ya wilaya yake.
Kwa upande wake diwani Chengula alisema uamuzi wa kunusuru uhai wa wagonjwa hao ulikuja baada ya wananchi wake kutoa taarifa na kuwa ataendelea kuwasaidia wagonjwa hao hadi watakapopona.
Chengula ambaye ameungana na mkuu huyo wa wilaya ya Iringa kukabidhi mahitaji mbali mbali zikiwemo nguo na mengine amejitolea kumsomesha motto wa darasa la tatu katika shule yake ya Sun Academy ambapo ada yake kwa mwaka ni zaidi ya shilingi milioni moja na kuwa atamlipia kwa miaka yote na kumwendeleza