Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Walemavu, Anthony Mavunde amesema kuanzia Julai Mosi, 2019 Serikali ya Tanzania itatoa tamko kuhusu ajira za madereva nchini humo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 26, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa kauli kuhusu malalamiko ya madereva wengi kutokuwa na mikataba ya ajira.
“Wamiliki wa malori walielezwa wazi wanapokwenda kusajili leseni Sumatra (Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri wa Majini na Nchi Kavu) waende na mikataba ya ajira ya wafanyakazi, ila siku mbili zijazo Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi ya Waziri Mkuu wataeleza hatua ambazo zimechukuliwa. Kila dereva atakuwa na mkataba wa kazi na litatolewa tamko,” amesema Mavunde.