Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WANAOSHITAKIANA KUGHARIMIA USAFIRI MABARAZA YA ARDHI


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amepiga marufuku wananchi wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi kutoa pesa kwa ajili ya kugharimia usafiri wa kwenda eneo lenye mgogoro.

Akizungumza wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki Dkt Mabula alisema, kutoa pesa ya kugharamia usafiri kwa mmoja wa wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi kwenda eneo la tukio kunaweza kuleta ushawishi kwa wajumbe wake hasa kwa yule aliyetoa kiasi kikubwa cha pesa.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, ni lazima wakati wa zoezi la kwenda eneo lenye mgogoro kwa wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri husika aratibu zoezi hilo huku ratiba nzima ikiwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya katika kipindi cha mwezi mmoja.

‘’ Jamaa anatoa laki mbili anayelalamika hana kitu unategemea hapo haki itatendekaje, ni marufuku kabisa na taratibu zote za kwenda uwandani zipitie kwa DC na ratiba ijulikane mapema’’ alisema Dkt Mabula.

Akigeukia uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba katika wilaya ya Ulanga, Dkt Mabula alisema Serikali imezindua Baraza hilo ili kupeleka huduma karibu na kurahisisha usikilizaji  kesi za ardhi kwa wananchi ambao baadhi ya maeneo wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo na kubainisha kuwa sasa wananchi wa Ulanga watapata  haki kwa wakati na kwa umbali mdogo.

Aliwaasa wananchi wa wilaya ya Ulanga kulitumia vyema Baraza Ardhi na Nyumba lililozinduliwa na kuwataka kuhakikisha wanafuata taratibu zote za utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na kuachana na ile migogoro ya kifamilia kwa kutumia Mabaraza ya Vijiji na Kata kushughulikia migogoro hiyo.

Dkt Mabula aliusifu mkoa wa Morogoro kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na kubainisha kuwa mafunzo hayo yawe chachu kwa wajumbe wake kutenda haki wakati wa kufanya maamuzi kwa kuwa tayari wana weledi katika eneo hilo.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo alisema, uzinduzi wa Barazala la Ardhi katika wilaya ya Ulanga limejibu kiu ya muda mrefu ya wananchi wa wilaya hiyo kupata huduma kwa ukaribu ambapo awali iliwalazimu kusafiri umbali mrefu hadi Kilombero kupata huduma.

Kwa mujibu wa Stela, kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga sasa kunaufanya mkoa mzima wa Morogoro kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Manne (4) na kubainisha kuwa Baraza hilo sasa linaongeza idadi ya Mabaraza yanayofanya kazi nchini kufikia 54 kati ya 97 yaliyoidhinishwa.

Msajili huyo wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini alisema, mkoa wa Morogoro pekee kwa sasa una Mashauri 2,500 ya ardhi kati ya 29,000 nchi nzima na kubainisha kuwa, kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga ni moja ya jitihada kuhakikisha Mashauri katika mkoa huo yanapungua kama siyo kuisha kabisa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com