Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATAJA MAMBO MATATU YANAYOSABABISHA AJALI ZA BARABARANI


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Imeelezwa kuwa moja ya chanzo kikuu cha ajali za barabarani hususan kwa waendesha bodaboda ni  makosa ya kibinadamu  ikiwa ni pamoja na ulevi na uzembe ambao huchangia kwa asilimia 76%.

Hayo yamesemwa leo Juni 13,2019 na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni wakati akijibu swali la mbunge wa  Musoma Mjini, Vedastus Mathayo Manyinyi aliyehoji  licha ya kazi nzuri ya waendesha bodaboda ya kurahisisha usafiri na kupunguza tatizo la ajira ,bado ziko changamoto mbalimbali wanazosababisha kama ajali za mara kwa mara pamoja na wizi  ,nini mkakati wa serikali kupunguza tatizo hilo. 


Katika majibu yake Mhandisi Masauni amesema vipo vyanzo vikuu vitatu vinavyosababisha ajali za barabarani hapa nchini ikiwa ni pamoja na makosa ya kibinadamu ambayo huchangia kwa asilimia 76%,ubovu wa Magari asilimia 16%, mazingira ya Barabara asilimia  8%. 


Mhandisi Masauni ameyataja baadhi ya makosa ya kibinadamu ni pamoja na ulevi,uendeshaji wa kizembe,mwendokasi,uzembe wa waendesha pikipiki,uzembe wa waendesha baiskeli,uzembe wa watembea kwa miguu. 


Aidha,Serikali kupitia jeshi la polisi hapa nchini imekuwa ikitoa elimu kwa waendesha bodaboda namna nzuri ya utumiaji wa pikipiki  ikiwa ni pamoja na kuvaa kofia ngumu ,kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa leseni kwa waendesha bodaboda  ili kupunguza  waendeshashaji  wasio na leseni  na wanaoweza kusababisha ajali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com