Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, amewataka wazazi nchini kutowaruhusu watoto wao kwenda kusherehekea Sikukuu ya Idd ufukweni (Beach), huku akitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kwa watakaokwenda kusherehekea kwenye maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Sheikh Salum kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi, alisema imekuwa kawaida kwa wazazi kuruhusu watoto kwenda kusherehekea sikukuu katika maeneo ya ufukweni jambo ambalo linaweza kuchangia hata maambukizi ya Ukimwi.
Alisema ifike wakati mamlaka zinazohusika ikiwamo Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua washerehekeaji ambao watakuwa wanatumia usafiri wa kukodi au binafsi kwenda katika maeneo hayo.
“Ninatoa wito kwa wazazi kuwazuia watoto wao kusherehekea sikukuu kwa namna hii, pia ninawaomba polisi kutumia nafasi zao kuwakamata wataokwenda kusherehekea ufukweni kwani huko ndiko wanakofanya maasi na kupoteza maana nzima ya sikukuu hii,” alisema Sheikh Salum.
Pia alisema kwa mwaka huu sherehe za Idd zitafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limetangaza sherehe ya Idd el Fitr kitaifa kwa mwaka 2019 itafanyika mkoani Tanga.
Limesema swala ya Idd itafanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Barabara ya 10, Ngamiani jijini Tanga kuanzia saa 1:30 asubuhi.
Baraza la Idd litafanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Social Plugin