TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi wanavyoendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa na ufadhili unaowezesha kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu nchini kwani uhalifu unaendelea kupungua na kuifanya nchi yetu kuendelea kuwa shwari na salama.
Yapo matukio mchache ambayo tunaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wananchi wote katika kupeana elimu ya kuyaepuka kuyatenda matukio kama vile mauaji yanayotokana na vitendo vya wananchi kujikulia sheria mikononi, wivu wa mapenzi na ulevi. Pia matukio ya ubakaji na ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva.
Jeshi la Polisi Tanzania lina amini kama kila mtu kwa nafasi yake akishiriki katika kutoa elimu, kuonya na kufiwachua wanaotenda uhalifu huo, kuanzia ngazi ya familia matukio ya aina hiyo yatapungua kwa kiasi kikubwa.
Mtakumbuka pia tarehe 01/06/2019 serikali ilitoa maelekezo kuwa, ndiyo mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini na utekelezaji ukaanza kwa ufanisi mkubwa. Jeshi la Polisi linatoa wito agizo hilo liendelee kuzingatiwa na wenye mifuko ya aina hiyo waisalimishe kama ilivyoelekezwa na kama kuna mwenye taarifa za mtu mwenye kumiliki mifuko hiyo atoe taarifa Polisi au mamlaka zingine ili hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni ziweze kuchukuliwa.
Aidha, kama mnavyofahamu tunaelekea kipindi cha sikukuu ya Eid El Fitri ambayo husheherekewa duniani kote baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watanzania wote kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama ili waweze kusheherekea kwa amani na utulivu sikukuu hiyo kubwa na muhimu.
Kila mmoja ajiepushe na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao kama vile kuacha nyumba bila waangalizi, ulevi wa kupindukia, kuruhusu vijana na watoto walio chini ya uangalizi wa wazazi kwenda katika nyumba za starehe au maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama na utu wao. Kujiepusha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama barabarani kama vile kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa , mwendo kasi, pamoja na kujaza abiria kupita kiasi.
Pamoja na kwamba, Jeshi la Polisi katika Mikoa yote limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya ibada na maeneo mengine ambayo yatakayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu tunaelekeza kila mmoja usalama uanzie kwake na kwa wale wanaomiliki maeneo ya starehe wazingatie maelekezo ya kiusalama waliopewa na
Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi na watakayoendelea kuwapa. Pia tunatoa onyo kwa wale wanaodhani wanaweza kutumia sherehe hizi kufanya uhalifu watambue kuwa watashughulikiwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za nchi.
Tunawaomba wananchi wote pale watakapoona viashiria au kumtilia mtu mashaka kuwa huenda akawa mhalifu watoe taarifa kupitia namba za simu za bure 0787 668 306 au 111 au 112.
Tunawatakia Watanzania wote Sikukuu njema yenye amani na utulivu ya Eid El Fitri.
Imetolewa na:
……………………………..
DAVID A. MISIME - SACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi.
Social Plugin