Kufuatia kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa Pasipoti Mpya za Kielektoniki (e Passport), Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha umma kuwa, tayari imekamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya utoaji wa huduma ya pasipoti hizo katika Mikoa ishirini na tisa (29), Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu, Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar na Ofisi za balozi za Tanzania Ishirini na tatu (23) zilizopo nje ya Nchi;
ambazo ni Uingereza (London), Ufaransa (Paris), Marekani (Washington DC na New York), Canada (Ottawa), Israel (Telaviv), Saudi Arabia (Jeddah na Riyadh), Comoro (Moron), Kenya (Nairobi na Mombasa), Ujerumani (Berlin), Algeria (Algiers), Italia (Rome), Nigeria (Abuja), Misri (Cairo), Uholanzi (The Hague), Ubelgiji (Brussels), Zambia (Lusaka), India (New Delhi), Malawi (Lilongwe), China (Beijing), Malaysia (Kuala Lumpur).
Nchi ambazo zitafunguwa Mfumo huo hivi karibuni ni Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe. Aidha, kwa Balozi zilizosalia, kazi ya ufungaji mitambo ya huduma hiyo inaendelea na itakamilika hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu.
Kwa Msingi huo, Idara ya Uhamiaji inawakumbusha Watanzania wote Ndani na Nje ya Nchi kuwa matumizi ya Pasipoti za zamani yatasitishwa ifikapo tarehe 31 Januari, 2020.
Aidha, idara inawasisitiza wale wote wenye Pasipoti za zamani (MRP) na wanaokusudia kusafiri nje ya Nchi hivi karibuni, kuhakikisha wanabadilisha Pasipoti zao mapema kabla ya mwezi Julai mwaka huu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wa kurejeshwa katika Viwanja vya Ndege na Vituo vya Mipakani wakati wa kutoka Nchini. Ni hitajio la Kisheria kwa Pasipoti kuwa na angalau uhai wa kuanzia miezi sita ili mwenye pasipoti hiyo aweze kuomba Visa ya Nchi anayokwenda na kuruhusiwa kuondoka Nchini kupitia Vituo vya kuingia na kutoka nchini.
Imetolewa na
Ally M. Mtanda (SI)
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji
Makao Makuu, Dar es Salaam
Social Plugin