Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YASAINI MKATABA WA KUPATIWA FEDHA ZA MSAADA BILIONI 60 KUTOKA SERIKALI YA CHINA


Tanzania imetia saini Mkataba wa kupatiwa fedha za Msaada wa Shilingi Bilioni 60 za kitanzania kutoka Serikali ya Watu wa China bila ya masharti yeyote ambapo Serikali ya Tanzania itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake.

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi  ambaye ameiwakilisha Serikali ya Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Bw. Zhou Liujun kwa upande wa Serikali ya China. Mkataba huo umesainiwa punde tu mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Waziri  Prof Palmagamba John Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi.

Mazungumzo ya Mawaziri hao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya China na Tanzania sambamba na  kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya China na Tanzania.

Maeneo hayo ni pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwa  Taasisi Mahiri ya Tiba ya Moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawatt 358) na Rumakali (megawatt 222) mkoani yaliyoko mkoani Iringa na Njombe ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580,pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway) sambamba na ukarabati wa reli ya TAZARA.

Aidha, katika mazungumzo yao, Serikali ya China imeahidi pia kuunga mkono katika ujenzi wa miundombinu muhimu katika mji mpya wa Serikali katika makao makuu Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China na mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi amesifu mahusiano mema na ya kirafiki baina ya Tanzania na China na kuongeza kuwa Tanzania imekuwa Rafiki wa kweli wa China kwa wakati wote.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya China sambamba na kueleza kuwa kipaumbele cha Tanzania ni kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia,kisaiasa na kiuchumi yaliyopo baina ya Nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pia Prof. Kabudi ameipongeza Serikali ya China na Nchi za Afrika kwa kuandaa mpango kazi wa kimkakati ambao umeanisha maeneo kumi ya kipaumbele yakiwemo uendelezaji wa sekta ya viwanda na miundombinu ambayo kwa nchi za Afrika hususan Tanzania ndio kipaumbele cha kwanza. Maeneo mengine ya kipaumbele ni pamoja na uendelezaji wa biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika pamoja na ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama kwa kutaja machache.

Halikadhalika, Prof Kabudi ameisifu Serikali ya China kwa kubainisha hatua kubwa nane zitakazosaidia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Beijing (2019 – 2021). Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha program maalum ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda (Industrial park), ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji na mawasiliano,mpango maalum wa ujenzi wa vyuo vya ufundi na vituo vya kutolea mafunzo ya stadi kwa ajili ya kuandaa nguvu kazi ya kufanya kazi viwandani.

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amehudhuria mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 53 za Afrika na taasisi za fedha za China ambazo ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo kati ya China na Afrika (CAD FUND), Benki ya Exim ya China pamoja Benki ya Maendeleo ya China yenye lengo la kutoa ufafanuzi na utaratibu wa fedha kiasi cha Dola bilioni 60 zilizoahidiwa na Serikali ya China wakati wa Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi za Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba, 2018 jijini Beijing.

Awali, katika ya ufunguzi wa mkutano huo,mchumi mkuu wa Benki ya Maendeleo ya China Liu Yong amesema China ina matumaini makubwa kuwa Afrika itaendelea kiuchumi na kwamba wataendelea kushirikiana na Nchi zote kwa kuwa malengo yao ni kuona nchi za Afrika zinaendelea kupitia ushirikiano baina ya China na Afrika.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
BEIJNG - CHINA.
24 Juni 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com