Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF(aliyesimama) akizungumza kwenye kikao kazi cha viongozi ,watendaji na wawezeshaji wa majaribio ya utambuzi wa Kaya za Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evold Mmanga (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao kazi cha viongozi ,watendaji na wawezeshaji wa majaribio ya utambuzi wa Kaya za Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika Mtwara.
Mtaalamu wa Mafunzo na Uwezeshaji wa TASAF Bi. Mercy Mandawa akitoa maelezo katika kikao kazi cha viongozi,watendaji na wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa majaribio ya utambuzi wa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Baadhi ya Washiriki wa kikao kazi cha kujenga uelewa wa uetekelezaji wa majaribio ya utambuzi wa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini (picha ya juu na chini).
Picha ya pamoja
*****
Na .Estom Sanga-Mtwara.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF umeanza mkakati wa kuwajengea uelewa viongozi ,Watendaji na Wawezeshaji katika ngazi ya halmashauri za Wilaya juu ya zoezi la utambuzi wa Kaya za Walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini ili kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa ufanisi mkubwa .
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi kilichofanyika mjini Mtwara, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,bwana Ladislaus Mwamanga amesema zoezi hilo linakusudia kuboresha mapungufu yaliyojitokeza kwenye sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango huo inayotarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuwa majaribio hayo ambayo kwa kiwango kikubwa yatatumia njia ya mfumo wa kompyuta yatafanyika katika Halmashauri za wilaya ya Siha,Mtwara na Tandahimba.
Bwana Mwamanga amesema baada ya kukamilika kwa majaribio hayo, kazi ya kutambua Kaya za Walengwa watakaojumuishwa kwenye Mpango itafanyika nchini kote ili kutekeleza maagizo ya Serikali ya kujumuisha maeneo yote kwenye shughuli za Mpango.
Katika Awamu ya Kwanza ya Mpango serikali kupitia TASAF imeweza kutekeleza Mpango huo kwa asilimia 70 ya mitaa/vijiji/shehia na hivyo asilimia 30 iliyosalia itakamishwa katika sehemu ya pili ya Mpango itakayotekelezwa kwa takribani miaka mitano ijayo.
Akifafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema mkazo mkubwa katika sehemu ya pili ya Mpango imewekwa zaidi katika kuhamasisha Walengwa wa Mpango kufanyakazi kwenye miradi ya Maendeleo watakayoiibua na kisha kulipwa ujira ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza adha ya umaskini.
“…tumeweka mkakati bora zaidi ya kutekeleza maagizo ya serikali ya kupunguza dhana ya Walengwa wa Mpango kuwa tegemezi” amesisisitiza bwana Mwamanga.
Amewahimiza Viongozi,Watendaji na Wawezeshaji kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenye mikutano ya utambuzi wa Kaya za Walengwa ili kuondoa uwezekano wa kaya zenye uhitaji kutojumuishwa kwenye Mpango na hivyo kuondoa manung’uniko baada ya kuanza kwa sehemu ya pili ya Mpango unaotarajiwa kuzifikia takribani Kaya milioni 1.3 ikilinganishwa na Kaya Milioni 1.1 zilizoandikishwa katika sehemu ya Kwanza.
Bwana Mwamanga amesema kutokana na usimamizi thabiti wa Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, kumekuwa na mafanikio makubwa kwa Kaya za Walengwa kuanza kuboresha maisha yao huku sehemu kubwa ya kaya hizo zikitumia fursa ya kuwemo kwenye Mpango kuanzisha shughuli uzalishaji mali jambo ambalo amesema limeendelea kuvutia Wadau mbalimbali wa Maendeleo kutaka kuchangia zaidi raslimali fedha na Utaalam.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara bwana Evold Mmanda amesema TASAF kwa kiwango kikubwa imekuwa kielelezo bora cha kuwafikia wananchi wanaoendelea kuishi katika mazingira ya umaskini kutokana na namna Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini walivyotumia fursa hiyo kupunguza athari za Umaskini.
Bwana Mmanda amewataka viongozi katika maeneo ya utekelezaji wa shughuli za Mpango kuendelea kuwahamasisha wananchi kuuchukia umaskini kwa vitendo jambo ambalo amesema linawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake.
Social Plugin