Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) YASEMA HAITATUMIA WAKURUGENZI KUSIMAMIA UCHAGUZI


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesisitiza vifungu vya sheria vilivyokuwa vikiruhusu wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na majiji kusimamia uchaguzi ambavyo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imevitengua, havitatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli hiyo ya NEC imekuja wakati kukiwa na sintofahamu, hasa baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga utekelezaji wa hukumu hiyo.

Katika hoja zake, AG alisema utekelezaji wa hukumu hiyo unasimama hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamriwa.

Hata hivyo, akizungumza katika mkutano wa NEC na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambao uandikishaji wake unatarajiwa kuanza Julai, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage alisema katika kutekeleza majukumu yao, vifungu hivyo vya Sheria ya Uchaguzi 7(1) na 7(3) havitatumika.

Mkutano huo ulifanyika jana katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Jaji Kaijage ambaye alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi aliyetaka kujua msimamo wa NEC baada ya mahakama kuondoa vifungu hivyo, alisisitiza pasipo kueleza kwa kina kuwa “vifungu vingine vya sheria hiyo ambavyo havikulalamikiwa vitaendelea kutumika kama kawaida”.

Pamoja na hayo, Jaji Kaijage  hakufafanua ni nani ambao watasimamia uchaguzi baada ya wao kuamua kutotumia vifungu hivyo.

Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu – Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo, ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa kuwa kinapingana na sheria mama, yaani Katiba.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akitetewa na Wakili Fatma Karume, pia mahakama hiyo ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

 Mahakama ilisema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao ambao si waajiriwa wa NEC, huteuliwa na rais aliyeko madarakani, ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Alisema kifungu cha 7(1) kinasema kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na sheria mama ambayo inasimamia nchi. Pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Jaji Ngwala alisema, lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote anayekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Mei 13, AG Dk. Kilangi alisema Serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi kwa niaba ya NEC.

Dk. Kilangi alisema tayari Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG) imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Alisema kuwapo kwa hukumu hiyo hakuathiri chaguzi nyingine zijazo, zikiwemo ndogo, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa itakapoamuliwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com