Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJENZI WA TAWI JIPYA LA IFM SIMIYU KUKAMILIKA SEPTEMBA 2019

Na Stella Kalinga, Simiyu

Makamu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta  amewahakikisha wananchi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kuwa ujenzi wa awali wa  tawi la Chuo hicho mkoani Simiyu ,unatarajia kukamilika  mwezi Septemba mwaka huu na kuanza kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo 2019/2020 .

Profesa  Satta ameyasema hayo Juni 17, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Tawi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Simiyu katika kijiji cha Sapiwi wilaya ya Bariadi.

Profesa  Satta  amesema kujengwa kwa kituo hicho kipya cha mafunzo kutachangia kuongeza udahili na  kubainisha kuwa katika mpango mkakati wa chuo mwaka 2016/2017 hadi mwaka 2020/2021, chuo kimejipanga kuongeza kutoa mafunzo kwa wateja wake hasa katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Simiyu inayotarajiwa kuchukua mikoa ya kanda ya ziwa mpaka Tabora.

Ameongeza kuwa azma ya chuo ni kuanza kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo 2019/2020 kuanzia ngazi ya cheti  na matarajio ni kuhamisha wanafunzi wa ngazi ya cheti na stashahada kutoka Mwanza kuja Simiyu ili Mwanza zibaki kozi za jioni wanazosoma watu wanaotoka kazini.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amempongeza Makamu Mkuu wa Chuo IFM, Prof. Tadeo Satta kwa kuwa mtendaji wa mipango aliyoipanga na kutimiza ahadi ya kuanza kujenga tawi hilo mwaka huu, huku akitoa wito kwa  wananchi wote kuchangamkia  fursa mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hosteli, migahawa na nyumba za kupangisha watumishi.

“Tawi la Chuo cha IFM linajengwa Sapiwi watu wote wanaalikwa kuchangamkia fursa na wachangamikiaji wa fursa wa kwanza ni wana Sapiwi wenyewe, tungehitaji kupata hosteli, migahawa ya chakula, maeneo ya watu kunywa vinywaji na tutawaambia TANROADS waone namna ya kuweka “stendi” maana hapa Sapiwi kitakuwa kituo kikubwa” alisisitiza Mtaka.

Aidha, Mtaka amewahakikishia viongozi wa Chuo cha IFM kuwa viongozi wa Mkoa wataendelea kushirikiana nao  katika kuhakikisha azma ya kukamilisha ujenzi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwezesha mkandarasi kufanya kazi saa 24 kwa kuhakikisha kuna ulinzi  na miundombinu ya umeme inakuwepo katika eneo la ujenzi.

Naye Mayunga Juma Mkazi wa kijiji cha Sapiwi amesema wananchi wa Sapiwi wanashukuru  uwepo wa ujenzi huo kwani umesaidia kutoa ajira na kuwawezesha kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi huo kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) Kagera,   Baluye Mitinje  ameahidi kusimamia na kuhakikisha ujenzi unafanyika usiku na mchana ili ukamilike kwa wakati.

Ujenzi wa awali wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha Tawi la Sapiwi utagharimu kiasi cha shilingi milioni mia tisa na sabini na moja .

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com