Umoja wa Afrika AU umechukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Sudan katika jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Afrika mpaka pale Baraza la Kijeshi litakapokabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Umoja huo pia umesema unajadili suala la kuwawekea vikwazo maafisa wa jeshi la Sudan waliohusika na mashambulizi dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imetolewa katika kikao cha dharura cha Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kinachokutana mjini Addis Ababa huko Ethiopia kwa ajili ya kutathmini hali ya mambo nchini Sudan.
Katika kikao hicho pia Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limelaani tena mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Sudan na kupinga mabadiliko ya aina yoyote yasiyokuwa ya kikatiba.
Msimamo huo wa Umoja wa Afrika umechukuliwa huku Baraza la Kijeshi lililotwaa madaraka nchini Sudan likiendelea kukabiliwa na upinzani mkali wa wananchi na vyama na makundi ya upinzani yanayosisitiza kuwa yataendelea kufanya maandamano na migomo ya kijamii hadi pale wanajeshi watakapokabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Waziri wa afya nchini Sudan amesema kuwa ni watu 46 pekee waliofariki katika ghasia za hivi majuzi, madai yanayopingwa na kamati ya madaktari nchini humo ambao wamesema kuwa idadi hiyo inafika watu zaidi ya 100.
Social Plugin