Tarehe 31 Mei, 2019, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea katika Uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata Thelathini na mbili (32) za Tanzania Bara. Uteuzi huo ulifanyika kama ilivyopangwa.
Katika Kata hizo Thelathini na mbili (32), jumla ya wagombea 98 kutoka katika Vyama kumi na nne (14) vya Siasa walichukua Fomu za Uteuzi. Vyama hivyo ni pamoja na AAFP, UMD, ADA – TADEA, CCK, CCM, CHADEMA, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, NCCR - Mageuzi, NRA, SAU, TLP, UDP na UPDP.
Hadi muda wa mwisho wa uteuzi tarehe 31 Mei, 2019 saa 10: 00 jioni kati ya wanachama 98 waliochukua fomu za uteuzi, 41 walirejesha fomu hizo, kati ya hao 27 walikidhi vigezo na kuteuliwa kuwa wagombea. Wanachama wengine watano (5) hawakuteuliwa kuwa wagombea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kurejesha fomu za uteuzi nje ya muda, kukosa uthibitisho wa malipo ya dhamana na wagombea kuwa na idadi pungufu ya wadhamini.
Jumla ya wagombea Watano (5) wa nafasi ya Udiwani waliwekewa pingamizi kwa Msimamizi wa Uchaguzi na hivyo kupelekea wagombea wawili (2) kuenguliwa kutoka katika orodha ya wagombea wa nafasi ya Udiwani.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea Rufaa moja (1) kutoka kwa Mgombea Udiwani wa Kata ya Ipole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Sikonge kupitia Chama cha Wananchi CUF, na malalamiko kutoka kwa wagombea wa CHADEMA na CUF katika Kata ya Murangi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Malalamiko yao ni dhidi ya maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi ya kuwaondoa kwenye orodha ya wagombea udiwani.
Tume katika kikao chake kilichofanyika leo tarehe 4 Juni, 2019 kimetoa maamuzi kama ifuatavyo:-
Kwanza, Tume imekubali rufaa moja ya mgombea Udiwani wa CUF katika Kata ya Ipole Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na hivyo kumrejesha kuendelea kuwa kugombea katika nafasi hiyo.
Pili, Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi katika Kata ya Murangi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ya kuwaondoa Wagombea wa CUF na CHADEMA katika orodha ya wagombea na hivyo Wagombea kuendelea kuenguliwa kugombea Udiwani.
Katika Uteuzi huu wa Udiwani katika Kata thelathini na mbili (32, jumla ya Wagombea udiwani katika Kata 29 wamepita bila kupingwa, na mgombea wa CUF kutoka Kata ya Kyaitoke Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na mgombea wa ACT –Wazalendo kutoka Kata ya Boma iliyopo katika Halmashauri ya Mji Mafinga wamejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, hivyo Kata moja (1) ndio itakayofanya uchaguzi hapo tarehe 15 Juni, 2019, kata hiyo ni Ipole Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Kampeni za uchaguzi zimeshaanza kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi na zitaendelea hadi tarehe 14 Juni, 2019 ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.
Taarifa zaidi kuhusu walioteuliwa inapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya www.nec.go.tz na Ofisi za Tume Makao Makuu.
Imetolewa tarehe 4 Juni, 2019.
Dr. Athumani Kihamia
MKURUGENZI WA UCHAGUZI