Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka viongozi wa Serikali mkoani Simiyu kuisaidia na kuilea Sekta Binafsi ili iendelee kukua na wahakikishe kuwa maamuzi wanayofanya hayawi vikwazo katika mazingira ya biashara na uwekezaji.
Mtaka ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya Utetezi na majadiliano katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani Simiyu ambayo imefanyika mjini Bariadi.
Amesema viongozi wa Serikali mkoani humo wanapofanya maamuzi katika biashara za watu ni lazima wawe na nia ya dhati ya kuona sekta binafsi inakuwa, ili maamuzi ya viongozi hao yasiwe vikwazo kwa ukuaji wa Sekta binafsi na mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Sekta binafsi ni lazima ilelewe anaeilea ni Serikali, Sekta binafsi ni lazima ilindwe anayeilinda ni Serikali,Sekta binafsi ni lazima isimamiwe anayeisimamia ni Serikali na Serikali inaisimamia kwa maana ya kuilea ili ifanye vizuri” alisema Mtaka.
Aidha, ametoa wito kwa Wakuu wa Wilaya mkoani Simiyu kuendeleza utaratibu wa kukutana na wafanyabishara ili kupata nafasi ya kujadiliana juu ya fursa mbalimbali za uwekezaji na namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akisisitiza pia kuendelea kufanyika kwa mabaraza ya biashara ya wilaya.
Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini(TCCIA) Mkoa wa Simiyu, Bi. Christina Matulanya amesema ili kuboresha mazingira ya biashara Serikali inapaswa kuendelea kuvutia wawekezaji na kusimamia sheria, sera na kanuni zisipindishwe, huku akiupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuandaa mwongozo wa uwekezaji.
Katika hatua nyingine Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu, Bw. Charles Mkumbwa ametoa wito kwa wafanyabiashara kuwa wazalendo, kutoa risiti ipasavyo, kufuata sheria za kodi na akaahidi kuwapa ushirikiano wafanyabiashara kila wanapohitaji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shule ya biashara, Khalidi Swabiri ambaye alikuwa mwezeshaji wa warsha hii amesema ni vema mabaraza ya biashara ya wilaya yakafanyika ili wafanyabiashara wapate muda wa kukutana na viongozi wa Serikali, sekta binafsi kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika mazingira ya biashara na uwekezaji na ufumbuzi wake.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini(TCCIA), Dkt. Meshack Kulwa amesema pamoja na kuomba mabaraza ya biashara ya wilaya yafanye kazi, ameomba TCCIA mkoani Simiyu itafute viongozi watakaofanya kazi kwa kujituma ili TCCIA Simiyu iweze kuwa imara.
MWISHO