Upinzani nchini Sudan umetangaza kufanya kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima kuanzia Jumapili (09.06.2019) hadi pale baraza la kijeshi la mpito litakapokabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Tangazo hilo lililotolewa na chama cha wanataaluma wa Sudan SPA, ambacho awali kilianzisha maandamano dhidi ya kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir aliyeondolewa madarakani, linakuja siku chache baada ya jeshi kuwashambulia waandamanaji na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha mjini Khartoum na hivyo kuvunja matumaini ya makabidhiano ya kidemokasia ya madaraka.
"Vuguvugu la uasi wa kiraia litaanza Jumapili na kukoma tu pale serikali ya kiraia itakapojitangaza yenyewe kupitia televisheni ya taifa", ilisema sehemu ya taarifa ya chama cha wanataaluma wa Sudan SPA.
Tamko lao linakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kukutana kwa nyakati tofauti na majenerali wanaotawala na viongozi wa waandamanaji katika juhudi za kufufua mazungumzo ambayo yalikaribia kuvunjika baada ya waandamanaji waliopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi kutawanywa siku ya Jumatatu.
Kamati kuu ya chama cha Madaktari wa Sudan, ambao ni moja ya makundi ya waandamanaji imesema kiasi cha watu 113 waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa tangu siku ya Jumatatu.
Inasema takribani miili 40 imeopolewa kutoka mto Nile mjini Khartoum na kuchukuliwa na vikosi vya usalama tangu kuzuka kwa ghasia.
Chama cha wanataaluma wa Sudan ambacho kiliongoza maandamano yaliyomuondoa Bashir, kimesema kinakubaliana na usuluhishi wa waziri mkuu Ahmed lakini kikatoa masharti kabla ya kurejea meza ya mazungumzo.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuanzishwa kwa tume huru itakayoungwa mkono kimataifa kwa ajili ya kuchunguza vurugu zote zilizojitokeza baada ya Al-Bashir kuondolewa mamlakani na kisha kuwachukulia hatua waliohusika.
Chama hicho pia kinataka kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa na kwamba mazungumzo ya upatanishi yajikite zaidi katika makabidhiano ya madaraka kwa serikali ya kiraia.
Social Plugin