Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE CHADEMA WATIMULIWA BUNGENI


Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson jana jioni aliwatoa ndani ya ukumbi wa Bunge wabunge watatu wa Chadema walioibua zogo bungeni kuhusu uamuzi uliochukuliwa dhidi ya mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana kitabu cha hotuba mbadala ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020.


Wabunge hao ni Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Dk Emmaculate Sware (Viti maalum), ambao walipinga uamuzi wa Dk Tulia kumtaka Vuma kuomba radhi kwa alichokuwa akizungumza wakati akichana kitabu hicho, si kitendo chake cha kuchana kitabu.

Dk Tulia alichukua uamuzi huo kwa maelezo kuwa taarifa iliyoombwa na mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka baada ya Vuma kuchana kitabu hicho, inazungumzia mbunge kutamka maneno yasiyoruhusiwa bungeni.

Vuma wakati akizungumza utekelezaji mzuri wa miradi ya Serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), alishika kitabu hicho cha upinzani na kusema kina maneno yasiyofaa na kinafaa kuchanwa kisha kukichana.

“Mchangiaji wakati akizungumza amechana hotuba ya upinzani ndani ya Bunge nafikiri jambo hili ni dharau kubwa. Ni kutojielewa kwa mbunge na hajui kwa nini vitabu hivi amepewa. Achukuliwe hatua maana tumemuona kama kichaa fulani hivi ndani ya Bunge,” alisema Mwakajoka aliyetumia kanuni ya 64 ya Bunge kutoa taarifa hiyo.

Katika majibu yake Dk Tulia alisema, “Ameitaja kanuni ya 64 japokuwa ufafanuzi wake haukuwa haswa katika kifungu gani ambacho kimevunjwa, kanuni hii inazungumzia mambo yasiyoruhusiwa bungeni na ukiisoma fasili ya kwanza inazungumza kuhusu kutotumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.”

“Kwa mchango wa Vuma hoja iliyopo itakuwa si kuchana kitabu maana amezungumza wakati akichana kitabu. Vuma maneno ya kuhusu kukichana kitabu nitakupa fursa ya kuyafuta na jambo hili lisirudiwe tena.”

Baada ya kupewa fursa hiyo Vuma alifuta maneno hayo na kusisitiza, “ila  ilikuwa ni kuonyesha namna gani ambavyo hotuba hii haina maslahi kwa umma.”

Kauli hiyo iliwanyanyua Heche na Matiko na kutaka mbunge huyo kuchukuliwa hatua zaidi.

“Waheshimiwa wabunge ndio maana huwa nasisitiza anapozungumza mmoja wetu kumsikiliza, Vuma ameonyesha kitendo ambacho mimi nimeshakitolea ufafanuzi, wakati amesema kitabu hiki kinapaswa kuchanwa. Vuma ameshaambiwa afute hayo maneno,” alisema Dk Tulia ambaye kabla hajamaliza wabunge wa upinzani walitaka achukue hatua zaidi.

“Naomba mtoke nje maana hatuelewani. Matiko na Heche namba mtoke nje. Matiko simama uende nje,” alisema Dk Tulia.

Dk Sware aliposimama na kutaka kutoa taarifa naye alitakiwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com