Wabunifu wa Ufundi Stadi, chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wamepata ufadhili wa jumla ya Shilingi 85 milioni kutoka kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wao.
Mkataba kwa ajili ya ufadhili huo umesainiwa jana tarehe 3 Juni 2019 katika ofisi za COSTECH jijini Dar es Salaam, kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu.
Ubunifu utakaopatiwa ruzuku ni “Pikipiki Salama” ya Mwl. Aneth Mganga wa Chuo cha VETA Kipawa, “Mashine ya Kufukuza Ndege Waharibifu Mashambani” ya Mwl. Emmanuel Bukuku wa Chuo cha VETA Dar es Salaam (Chang’ombe) na “Kifaa cha Kufundishia Elimu ya Mfumo wa Jua na Sayansi ya Anga” cha Ndg. Ernest Maranya, Mbunifu na Mhitimu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema VETA imebeba jukumu la kuwasimamia na kuwadhamini wabunifu hao na kwamba Mamlaka hiyo itahakikisha ubunifu huo unakamilika na kuingia sokoni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Baada ya kupokea ufadhili huo, mmoja wa wabunifu hao, Mwl. Emmanuel Bukuku, amesema kuwa anaamini ruzuku hiyo itamsaidia kuboresha ubunifu wake na kuhakikisha kifaa chake cha kufukuza ndege waharibifu mashambani kinaingia sokoni na kuwasaidia wakulima kulinda mazao yao mashambani na hatimaye kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Naye Mwl Aneth Mganga alisema kuwa ruzuku hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo anatamani kuboresha ubunifu wake wa “Pikipiki Salama” ili kusaidia kupunguza athari za ajali za barabarani kwa watumiaji wa pikipiki na wizi wa pikipiki, hasa zile zinazotoa huduma ya usafiri wa kibiashara (maarufu kama bodaboda). Ajali hizo zimekuwa zikisababisha vifo au ulemavu kwa vijana wengi nchini.
Kwa upande wake Ndg. Ernest Maranya ameishukuru COSTECH na VETA na kusema kuwa ruzuku hiyo itamsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya maboresho muhimu kwenye kifaa chake na kutatua changamoto iliyokuwa ikimkabili ya gharama za uagizaji wa malighafi nje ya nchi iliyosababishwa na ufinyu wa fedha.
Amesema kuwa kifaa hicho kikikamilika kitakuwa msaada mkubwa katika kufundisha elimu ya mfumo wa jua na sayansi ya anga, hasa kwa elimu ya msingi na sekondari. Ametoa wito kwa wabunifu wengine kujitokeza na kusajili bunifu zao ili wale watakaokidhi vigezo waweze kunufaika na ufadhili kama huo wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia COSTECH.