Sheikhe mkuu wa Mkoa wa Kagera Alhaji Kharuna Kichwabuta akimshukuru mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti Mara baada ya kumkabidhi shilingili milioni 2.1
Na Ashura Jumapili -Bukoba
Viongozi wa taasisi za dini ya Kiislamu Mkoani Kagera wameshauriwa kujiunga na kuwa pamoja katika kuleta maendeleo ya waumini wa dini hiyo na jamii inayowazunguka na kuacha tofauti zao.
Ushauri huo umetolewa na Sheikhe wa Mkoa wa Kagera Alhaji Kaharuna Kichwabuta katika hafla ya uzinduzi wa mpango mkakati wa maendeleo wa miaka mitano ulioandaliwa na taasisi ya Bakwata Mkoani humo Juni 22 mwaka hii katika viwanja vya shule sekondari Nyashenye wenye kauli mbiu" Bakwata Mpya Kagera,Nguvu moja kwa pamoja"
Alhaji Kichwabuta alisema katika kuujenga na kuutetea uislamu waislamu wenyewe wanatakiwa kuwa wamoja na kuutanguliza uislamu wao kwanza kabla ya mambo mengine.
Aliwaomba viongozi wa taasisi nyingine kuunga mkono mpango huo na kutoa onyo kali kwa yeyote atakayejaribu kuukwamisha mpango huo kuwa hata kama atakuwa Sheikhe au kiongozi yeyote ndani ya Bakwata hatavumiliwa.
Katibu wa Bakwata Mkoa wa Kagera Abdumaliki Mwijage,akisoma lengo la mpango huo alisema mpango huo hauwezi kufanikiwa kama waislamu na wadau wengine hawatauunga mkono.
Mwijage,alimuomba mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti,kuwaomba wakuu wa wilaya zote kutoa ushirikiano pale watakapofatwa.
Pia alimuomba kuzisihi baadhi ya idara kuwaondela vikwazo pale wanapokwenda kuhitaji usaidizi wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Kwaupande wake mjumbe wa baraza la maulamaa Taifa Sheikhe Ally Mgeliko,alisema mpango huu unalenga hasa huduma za kijamii zikiwemo shule huduma za afya na mambo mengine hivyo waislamu wanatakiwa kuunga mkono kwa hali na Mali katika kutekeleza mpango huo mahususi kwa jamii.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Brigedia Jenerali Gaguti ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Kagera ,alisema ofisi take ipo wazi muda wote kwaajili ya kuwahudumia waislamu na jamii nzima ya Kagera.
Alisema mpango huu sio wa Bakwata bali ni wa wanakagera wote hivyo atahakikisha ana ulinda na wale wote wataoukwamisha watakuwa maadui wa Kagera.
Mkuu huyo wa Mkoa alikabidhi kiasi cha shilingi milioni 2.1zilizotolewa na osifi yake pamoja na wakuu wote wa Wilaya za Mkoa huo katika kuunga mkono mpango huo.
Alisema ili mkoa wa Kagera uwe na amani viongozi wa dini wanatakiwa kuhubiri suala la amani katika maeneo yao ili kuwajengea waumini wao kuwa na hofu ya mungu.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa jukumu langu la kwanza ni kuhakikisha amani na usalama katika Mkoa wangu lakini kuhakikisha wananchi wangu nawaletea maendeleo, hivyo mpango huu sio mpango wa Bakwata bali ni mpango wangu japo Bakwata wameonesha njia, niahidi kuulinda na kuhakikisha unafanikiwa kwa muda uliopangwa tena ikiwezekana kabla ya muda.” Amesema Gaguti.
Baadhi ya viongozi wa taasisi wameshukuru mpango huu endapo utatekelezwa kwa namna ulivyopangwa utasaidia jamii nzima ya Kagera na kuwataka viongozi kutoa elimu kwa kina kwa waumini juu ya mpango huu ili kuufanikisha kwa weledi na haraka.