OFISI YA KIJIJI YATUMIKA KAMA WODI YA KUJIFUNGULIA AKINA MAMA WAJAWAZITO


Jengo ambalo ujenzi wake umekwama kutokana na kukosekana fedha.Jengo hili ni kwa ajili ya zahanati ya kijiji cha Nkung'ungu ambayo kwa sasa huduma zinalazimika kutolewa katika ofisi ya kijiji (Picha na Joachim Nyambo).
**
Matumizi ya jengo lisilo rasmi katika utoaji wa huduma za afya katika kijiji cha Nkung’ungu wilayani Chunya mkoani Mbeya yametajwa kuhatarisha afya ya watoto wachanga na mama wajawazito wanaokwenda kujifungua.

Kutokana na kukosekana kwa jengo lenye kukidhi tija,huduma za Zahanati ya kijiji cha Nkung’ungu wilayani Chunya zinalazimika kutolewa kwenye jengo la Ofisi ya kijiji ambalo ni chakavu kutokana na kuwa la miaka mingi.

Kati ya vyumba vilivyokithiri kwa ubovu ni pamoja na kinachotumika kuzalishia mama wajawazito ambacho licha ya kuwa na nyufa kubwa kwenye kuta zake pia bati za paa lake zimeoza na kusababisha matundu huku chumba hicho pia kikiwa na giza totoro.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea Zahanati hiyo,Muuguzi Joyce Mwambeme ambaye ndiye mtaalamu pekee alisema walilazimika kuhamia kwenye ofisi ya kijiji baada ya jengo la Zahanati kufungiwa kwa kukosa sifa kutokana na uchakavu mkubwa.

Joyce alisema changamoto kubwa ya jengo wanalotumia hivi sasa ni finyu hatua inayosababisha kuwepo na mlundikano wa vitu mchanganyiko ikiwemo madawa na vifaa tiba jambo lisiloweza kutofautisha eneo wanalotolea huduma na ghala.

Alisema huduma za mama wajawazito na watoto wachanga wanaozaliwa hapo zipo hatarini zaidi kutokana na chumba kinachotumika kutokidhi vigezo ambapo alisema kati ya athari zinazoweza kujitokeza kwa watoto wachanga ni pamoja na kuugua mafua na kikohozi kutokana na chumba hicho kuwa vumbi litokanalo na sakafu ya udongo.

Muuguzi huyo alisema hali ni mbaya zaidi pale inapotokea mvua inanyesha huku wakiwa kwenye wakati wa kumsaidia mjamzito kujifungua kwakuwa maji ya mvua hutiririkia hadi kwenye kitanda kutokana na ubovu wa paa.

“Mama mjamzito anapokuja kujifungua hapa sala ya kwanza tunayoomba ni mvua isije,maana huwa tunapata wakati mgumu mnooo….kama unavyoliona hili paa letu,lina matundu mengi na halifai kwa kweli.”

“Suala la mwanga nimekuwa nikilazimika kutumia tochi wakati wa kutoa huduma kwa wajawazito iwe usiku au mchana…maana kama unavyoona muda huu ni mchana lakini mwanga hautoshi hivyo lazima nitumie tochi wakati wa kumhudumia mama au mtoto”,alisema Joyce.

Alisema uchakavu wa chumba hicho unaweza kusababisha pia athari za vichomi kwa watoto wachanga kutokana na baridi kali inayokuwepo hususani katika msimu huu wa baridi.

Alibainisha kuwa zahanati hiyo isiyo rafiki ambayo hupokea wagonjwa wasiopungua 20 kwa siku,imekuwa pia ikipokea wajawazito wasiopungua 10 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nkung’ungu Essau Salima alisema jitihada zinazofanywa hivi sasa ni ujenzi wa jengo la zahanati ambao umekwama kutokana na nguvu za wananchi waliokuwa wakichangiwa kuelemewa.

Afisa Mtendaji wa kata ya Nkung’ungu,Osward Handula alisema ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa huduma za afya zinatolewa ndani ya jengo la ofisi ya kijiji hatua iliyolazimu shughuli za Mwenyekiti wa kijiji kuhamishiwa ofisi ya Kata hiyo.

Handula alisema hawakuwa na namna nyingine baada ya mamlaka za juu kuwafungia zahanati iliyokuwepo awali kwa madai ya uchakavu wa jengo uliopindukia na ndiyo sababu wakaomba na kupewa kibali cha kuendelea kutoa huduma za afya kwenye jengo la Ofisi ya kijiji linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi CCM.

Alisema uchakavu wa jengo hilo linalotumika kwa sasa unatokana na kuwa la zamani ambapo miaka ya nyuma enzi za ujamaa lilikuwa likitumika kama Duka la ujamaa.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya,Dk Felista Kisandu anasema jambo la kwanza alilolifanya mara baada ya tu ya kuhamia wilayani hapa miezi kichache iliyopita ni ziara ya kutambua Zahanati zote na vituo vya Afya vilivyopo.Kati ya maeneo aliyoshuhudia uwepo wa changamoto kubwa ni pamoja na kijiji cha Nkung’ungu.

Anasema anatambua jitihada zinazofanywa na wadau wakiwemo wananchi wanaohangaika kutafuta ufumbuzi kwa kujenga jengo litakalotumika kwaajili ya zahanati.

“Ni kweli changamoto hii ipo,nilikwishafika na kujionea mwenyewe.Nilikuwa kwenye ziara ya kuvitambua vituo vya afya na zahanati zilizopo wilayani hapa.Ni changamoto kubwa kwa kweli.Lakini katika suala la uhaba wa watumishi niseme jambo ambalo liko nje ya uwezo wangu.Nikisema namwachia mwajiri wangu nay eye anaweza kukujibu pia liko juu ya uwezo wake kwakuwa linahitaji kudra za kutoka juu”

Hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Mbeya,Rais Dk John Magufuli alipozungumza na wakazi wilayani Chunya aliitaja wilaya hii kuwa na changamoto ya Maeneo ya utoaji huduma za Afya ikiwemo ukosefu wa Hospitali ya wilaya yenye sifa licha ya kuwa ni wilaya Kongwe.

Na Joachim Nyambo,Chunya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post