Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WILAYA YA CHEMBA WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

 Muuguzi Msaidizi na Mkunga wa Zahanati ya Kata ya Sanzawa katika Halmashauri ya Wilaya Chemba mkoani Dodoma, Dativa Kiabuka akipokea boksi lenye dawa kutoka kwa Dereva wa Bohari ya Dawa (MSD), Marwa Peter Wangwe walipo pelekewa dawa hizo wilayani humo jana.
 Dereva wa Bohari ya Dawa (MSD), Marwa Peter Wangwe (wa pili kushoto) , akikabidhi dawa kwa kamati ya afya ya Kijiji cha Sanzawa. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa zahanati hiyo, Iddi Degera, Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kijiji hicho, Flaviana Joseph na Muuguzi Msaidizi  wa Zahanati hiyo, Dativa Kiabuka.
Muuguzi Msaidizi  wa Zahanati hiyo, Dativa Kiabuka, akisaini fomu maalumu baada ya kupokea dawa kutoka MSD.
 Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Sanzawe
 Mkazi wa Kijiji cha Moto, Ali Tengeneza, akizungumza.
 Mkazi wa Kata ya Sanzawa, Nicholaus Dominick, akizungumza.

 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Mkoa wa Dodoma, Innocent Mugisha, akikagua moja ya boksi la dawa katika chumba cha kuhifadhia dawa cha zahanati hiyo. Kulia ni Muuguzi wa zahanat hiyo, Dativa Kaibuka.
 Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kijiji hicho, Flaviana Joseph, akizungumza.
 Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sanzawa, Shabani Msemule akizungumza.


Na Dotto Mwaibale, Chemba Dodoma

WANANCHI wa Kata ya Sanzawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wameipongeza Serikali kwa kuboresha huduma za afya kuwapelekea dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa wakati jambo ambalo limewaondolea usumbufu wa kupata matibabu wanapoumwa.

Pongezi hizo walizitoa kwa nyakati tofauti wilayani humo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD), ambao wanawatembelea wateja wao katika vijiji vya Mkutimango na Minyembe kujua changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Mkazi wa Kijiji cha Moto, Ali Tengeneza alisema anaipongeza MSD na Serikali kwa kufanikisha kuwafikishia dawa kwa wakati tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakilazimika kwenda kuzinunua katika maduka ya watu binafsi.

" Watu katika familia yangu wakiumwa huwa nawaleta kutibiwa katika Zahanati yetu hii ya Kijiji cha Sanzawa na hakuna siku waliyokosa dawa " alisema Tengeneza.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sanzawa, Shabani Msemule alisema hapo awali walikuwa na changamto ya upatikaji wa dawa lakini hivi sasa haipo na dawa zinapo kuwa zimekwisha katika zahanati hiyo huwa wanakwenda kutibiwa Kituo cha afya cha Kwamtolo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa zahanati hiyo, Iddi Degera alisema hivi sasa hakuna changamoto ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati hiyo dawa na mahitaji mengine yanayohusu afya yanapatikana.

Mkazi mwingine wa Kata hiyo, Nicholaus Dominick aliiomba serikali kuboresha zaidi miundombinu ya zahanati na vituo vya afya.

Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kijiji hicho, Flaviana Joseph alisema mara kwa mara wamekuwa wakipokea dawa kutoka MSD na kuzipokea kwa utaratibu uliopo na orodha ya dawa zote wanazozipokea na thamani yake hubandikwa kwenye ubao wa zahanati hiyo ili kila mwananchi aweze kuona.

Muuguzi Msaidizi na Mkunga wa zahanati hiyo, Dativa Kiabuka alisema dawa zote muhimu wamekuwa wakizipata kwa wakati na hawajawahi kupungukiwa kutokana na utaratibu waliojiwekea wa kutoa oda pale wanapoona zinapungua na kuwa katika eneo hilo magonjwa yanayosumbua zaidi ni malaria,kukooa na matumbo na kuwa wagonjwa wanaotibiwa ni kuanzia 20 hadi 50 kwa siku.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com