Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAODAIWA KODI YA PANGO WAITWA OFISINI KWA LUKUVI BILA KUKOSA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atakutana na taasisi na mashirika ya umma 207 yanayodaiwa kodi ya pango la ardhi katika kikao maalumu ikiwa ni mkakati wa wizara hiyo kuhakikisha wadaiwa wa kodi hiyo wanalipa kwa mujibu wa sheria.


Wadaiwa watakaoshindwa kufika katika kikao hicho hatua za kufuta miliki zao na kuuza maeneo husika zitafuata kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura Namba 113 Kifungu cha 50.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika, Waziri atakutana na mashirika na taasisi hizo ukumbi wa Hazina Dodoma Juni 11, mwaka huu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, taasisi, mashirika na wenye viwanda na maeneo makubwa ya biashara ambao wana malimbikizo makubwa ya kodi ya pango la ardhi watatakiwa kufika katika kikao hicho maalum bila kukosa na nyaraka za umiliki na stakabadhi za malipo ya kodi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wadaiwa watakaoshindwa kufika katika kikao hatua za kufuta miliki zao na kuuza maeneo zitafuata.

Baadhi ya taasisi na mashirika yaliyopewa wito wa kuhudhuria kikao hicho ni Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), Bodi ya Pareto.

Nyingine ni Chuo cha Madini, Bodi ya Korosho, BP Tanzania Ltd, Puma Energy, Chuo cha Ushirika, CRDB, Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA), Kahama Mining Corporation na Kituo cha Elimu Kibaha.

Mengine ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Rubada-Wizara ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Pia zimo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Capco Tanzania Ltd, Aga Khan Foundation, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Exim Bank Tanzania na Shirika la Masoko Kariakoo.

Uamuzi wa kukutana na wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi ni mwanzo wa jitihada za kuhakikisha wadaiwa wa kodi ya ardhi wanalipa kodi hiyo kabla ya Juni 30, mwaka huu. Baada ya hapo watakaokaidi watafikishwa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya husika ambapo adhabu yake ni kufuta miliki na kuuza maeneo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com