Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJI UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA KUKAMATWA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangapo amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Kalambo pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama ya Wilaya kuwasaka na kuwatia nguvuni wananchi wanaosadikiwa kuhujumu miundombinu ya maji katika Kijiji cha Kisongamile ambacho kipo jirani na ujenzi unaoendelea wa hospitali ya wilaya ya kalambo hali inayopelekea kurudisha nyuma kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Amesema kuwa hospitali hiyo ni ya kwao na kwamba wao ndio wa kwanza kufaidika na ujenzi wa hospitali hiyo pindi itakapokamilika, hivyo amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha analimaliza tatizo hilo ndani ya muda mfupi ili kuendana na ratiba ya umaliziaji wa ujenzi wa hospitali hiyo.

“Nimeona hii changamoto ya maji pamoja na kwamba wanachimba kisima, lakini kile Kijiji pale ambacho kinakwamisha kinahujumu miundombinu ya maji Mhe. DC pamoja na kamati ya usalama muende pale, pamoja na mwenyekiti wa halmashauri, mkazungumze na kile Kijiji, lakini pia kama kuna watu ambao wanadhaniwa wanahujumu kwa makusudi miundombinu, haiwezekani Kijiji kizima kikawa kinahujumu miundombinu, mchukue hatu ya kuwakamata hao wote wanaohujumu miundombinu ya maji,” Alisisitiza.

Aidha, alieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa hoapitali hiyo ambapo mpaka tarehe 8.6.2019 bado wapo katika hatua ya kuweka kenchi na huku hawajaanza kuweka plasta wala kununua vifaa vingine kama milango, madirisha, vigae na mabomba na hivyo kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha wananunua vifaa hivyo mapema ili inapofikia hatua ya kuvipachika vifaa hivyo kusiwepo na usumbufu.

Halikadhalika amewataka mafundi wanaosimamia majengo ya hospitali hiyo kuhakikisha wanapiga plasta majengo yote na kutahadharisha kuwa fundi yeyote atakayepitisha muda wake bila ya kumaliza jengo itambidi fundi huyo kuilipa serikali na kusisitiza kuwa serikali haitaongeza hata siku moja katika kuhakikisha majengo hayo yanakamilika.

Ameyasema hayo alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo inayotakiwa kukamilika ifikapo tarehe 30.6.2019 akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na wataalamu kutoka katika ofisi yake.

Awali akielezea changamoto ya kusuasua kwa upatikanaji wa maji katika eneo hilo la ujenzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Msongela Palela alisema kuwa miongoni mwa changamoto kubwa ni uhujumu wa miundombinu ya maji inayoelekea kwenye ujenzi wa hospitali hiyo unaofanywa na wananchi wa Kijiji cha Kisongamile huku sababu kubwa ya uhujumu huo ni Kijiji hicho kukosa umeme.

“Changamoto nyingine ni ya hawa wenzetu wa Kijiji cha Kisongamile, ambao wao wanasema kwamba walipaswa kuwa wamepata umeme ambao mpaka sasa hawana umeme, kwahiyo kwasababu hiyo hii miundombinu ya maji wataendelea kuihujumu mpaka pale watakapokuwa wamepatiwa umeme, tunaendelea kuwaelimisha na kukaa nao kuwashauri kwamba wanachofanya ni hujuma kwa serikali yao lakini nimshukuru mkuu wa Wilaya ameshachukua hatua za awali kwamba wanaohujumu watambuliwe na kuchukua hatua,” Alisema

Pia, alisema kuwaendapo wananchi hao hawatadhibitiwa huenda wakati zitakapoanza opereshi za hospitali chnagamoto hiyo ikajitokeza hivyo ili kuhakikisha kwamba tahadhari inachukuliwa na kuwa hospitali inakuwa na maji wakati wote ndio maana tunakwenda kwenye wazo mbadala la kuchimba kisima.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya ya Kalambo Dkt. Allen Kalekwa wakti akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa hospitali hiyo alisema kuwa baadhi ya vifaa kwaajili ya umeme, bati na mbao za kenchi zimeshanunuliwa na vingine vipo njiani na kuwa hadi kufukia hatua hiyo tayari halmashauri imeshatumia shilingi milioni 940 na kubakiwa na shilingi milioni 560 ambazo ni kwaajili ya kununua vifaa kama, marumaru, aluminian, gypsum na fedha ya mafundi na kisha kueleza changamoto ya maji.

“Changamoto kubwa tuliyonayo kwa sasa ni tatizo la maji, tulishafunga mfumo wa maji mpaka hapa yalikuwa yanakuja lakini bahati mbaya kuna baadhi ya sehemu wanakata mabomba ya maji, lakini hatua za awali mpaka sasa hivi tumeshanunua madumu matatu ya lita 15,000 ya kuhifadhia maji na wenzetu wa ujenzi wa barabra wanatusaidia kutujazia maji lakini pia tunatarajia kuchimba kisima kwaajili ya utatuzi wa muda mrefu,” Alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com