Serikali imewafikisha mahakamani watu wanne kujibu shtaka la kuchapisha maudhui katika mtandao wa YouTube bila kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Washtakiwa hao ni Charles Kombe (24) mkazi wa Mikocheni, John Chuwa (28), mkazi wa Baracuda, Amos Warema (27) na Raymond Mkoroka (30). Walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Walisomewa mashtaka hayo mbele ya mahakimu mkazi wanne tofauti; Maira Kasonde, Janeth Mtega, Agustina Mbando na Augustine Rwizile.
Inadaiwa washtakiwa hao walichapisha mtandaoni maudhui hayo katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2018 na Mei mwaka huu, Dar es Salaam.
Mshtakiwa Kombe alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mbando ambapo Wakili wa Serikali, Elizabert Mkunde alidai alitenda kosa hilo kati ya Agosti mosi 2017 na Mei 21 mwaka huu katika maeneo tofauti Dar es Salaam.
Ilidaiwa alichapisha maudhui hayo kupitia mtandao wake wa YouTube uitwao Charles Kombe bila kibali.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka na imedaiwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Kombe yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na wadhamini wawili waliosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 5 kila mmoja. Kesi iliahirishwa hadi Julai 7, mwaka huu itakapotajwa.
Mshtakiwa Chuwa alisomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Kasonde na Wakili wa Serikali, Elizabert Mkunde.
Ilidaiwa alitenda kosa hilo katika terehe tofauti kati ya mwaka 2018 na Aprili 2019 Dar es Salaam.
Mshtakiwa anadaiwa kuchapisha maudhui kupitia mtandao wa Youtube uitwao John Film Entertainment bila kibali kutoka TCRA.
Alikiri kutenda kosa hilo na aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kujidhamini mwenyewe kwa dhamana ya maandishi ya Sh milioni 5 pamoja na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya kiasi hicho cha fedha.
Kesi iliahirishwa hadi Juni 7 mwaka huu mshtakiwa atakaposomewa hoja za awali.
Mshtakiwa Warema ilidaiwa kuwa alitenda kosa hilo kati ya Novemba 2018 na Mei 17 mwaka huu katika maeneo tofauti Dar es Salaam.
Alisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mtega na Wakili wa Serikali, Candid Nasua.
Anadaiwa alisambaza maudhui hayo kupitia mtandao wa Youtube uitwao Pro Media Tanzania bila kuwa na kibali kutoka TCRA.
Baada ya kusomewa, alikana shtaka hilo na aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kujidhamini na kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 3.
Kesi iliahirishwa hadi Julai 4, mwaka huu na upelelezi haujakamilika.
Mshtakiwa Mkoroka alisomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Elia Athanas mbele ya Hakimu Mkazi Rwezile.
Ilidaiwa alitenda kosa hilo katika tarehe tofauti jijini Dar es Salaam na alikana shtaka.
Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja na kujidhamini mwenyewe kwa kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 5. Kesi iliahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu itakapotajwa.