SALVATORY NTANDU
Serikali Mkoani Shinyanga imewataka wakurugenzi wa Halmashauri sita za mkoa huo kuhakikisha wanaweka Madirisha maalumu ya kutolea huduma za afya kwa wazee katika Zahabati, Vituo vya afya na Hospitali za Wilaya ili kuondoa malalamiko yanayotolewa juu ya upatikanaji wa tiba.
Uamuzi huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Tellack katika mkutano wa hadhara na wananchi uliokuwa na lengo la kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika kata ya majengo mjini Kahama baada ya kupokea malalamiko ya wazee juu ya kukosa huduma za afya.
Amesema Wazee kupatiwa huduma za afya bure ni hitaji la kisheria kwa wenye umri kuanzia miaka 60 ,hivyo wanapaswa kuhakikisha kila mzee mwenye umri huo anakuwa na kitambulisho maalumu kitakachomuwezesha kuapatiwa matibabu bure bula kusumbuliwa na wahudumu wa afya.
Amefafanua kuwa ni lazima wahakikishe wanapatiwa matibabu pamoja na dawa, pamoja na kuwepo kwa wahuduma maalumu ambao watakuwa wakiwasiliza matatizo yao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwao na kutowachanganya na makundi mengine ya wagonjwa.
Mbali na hilo Tellack amesema, serikali imetoa shilingi Bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 11 katika Halmashauri sita zilizopo katika mkoa wa Shinyanga ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kupambana na vifo vya akinamama wajawazito na watoto.
Amesema jukumu la kupambana na vifo vya akinamama wajawazito na watoto ni jukumu la kila mmoja hivyo ni budi wanaume wakawahimiza wake zao kujifungulia katika zahanati na vituo vya ili kuzuia vifo visivyo vya lazima.
Amefafanua kuwa upatikanaji wa dawa katika Hospitali, zahanati na vituo vya afya katika Mkoa wa shinyanga zinapatikana kwa asilimia 95 nakudai kuwa dawa ambazo utazikosa katika zahanati zitapatikana katika vituo vya afya au Hospitali za Wilaya.
Social Plugin